Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari KITU MUHIMU SANA UNACHOHITAJI ILI KUFANIKIWA…
Siyo akili, kwa sababu kila unachotaka kujua unaweza kujifunza.
Siyo kipaji, kwa sababu kila mtu kuna kitu anaweza kufanya vizuri zaidi.
Siyo bahati, kwa sabau bahati huwa hazitokei tu, zinatengenezwa.
Na siyo juhudi, maana wengi wanaweka juhudi lakini hawapigi hatua.
Unapotaka kufanikiwa kweli, unapotaka kutoka hapo ulipo sasa na kwenda mbele zaidi,
Unapotaka kufanya makubwa kwenye maisha yako,
Unahitaji kitu kimoja muhimu sana.
Ukikosa kitu hicho, hata kama utakuwa na juhudi kiasi gani, juhudi hizo zitazidi kukupoteza,
Hata kama utakuwa unajua kiasi gani, kujua kwako kutazidi kukuumiza.
Kitu muhimu sana unachohitaji ili kufanikiwa, ambacho ndiyo kitakuwezesha kupiga hatua ni NIDHAMU.
NIDHAMU ni muhimu mno, mno, nirudie tena, nidhamu ni muhimu sana kwa mfanikio yako.
Kupanga kila mtu anaweza kupanga,
Kusema ndiyo kabisa, kila mtu anasema sana,
Ila kukaa chini na kufanya kila siku, KILA SIKU, iwe ni siku ya raha kwako au siku ya huzuni, iwe ni siku jua limewaka au mvua imenyesha, iwe ni siku ya kazi au siku ya sikukuu,
Unahitaji kufanya kila siku.
Na kama huwezi kufaya kile ulichopanga kufanya,
Kama huwezi kusema hapana kwa dunia,
Kama kila wakati unayumbishwa na kila kinachoendelea,
Utaendelea kuwasindikiza watu kwenye hii safari ya mafanikio.
Haijalishi unayataka mafanikio kiasi gani, hutayapata.
Jijengee nidhamu, panga kufanya na fanya kweli, na inapofika wakati wa kufanya na ukataka kuahirisha, jikumbushe umuhimu wa kufanya.
Ukawe na siku bora sana ya leo rafiki, siku ya kufanya kweli, siku ya kuepukana na kelele zisizochangia ndoto yako.
#NidhamuMsingi, #Fanya, #NiLeoTu, #IngiaMzimaMzima #Mara10
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha