Katika mambo kumi uliyopanga kufanya leo, mawili mpaka matatu ndiyo muhimu zaidi.
Hii ina maana kwamba ukifanya hayo matatu, ukayafanya vizuri, huna hata haja ya kufanya yale 7 yaliyobakia. Kwa sababu umehimu wa mambo hayo matatu ni mkubwa kuliko yale mengine saba.
Pamoja na hili, watu wamekuwa wanakazana kufanya mambo yote kumi waliyopanga kufanya, wanayafanya kwa kiwango cha chini sana na mwishowe wanashindwa kupata matokeo mazuri kwenye jambo lolote.

Ufanisi haimaanishi kufanya kila kitu unachoweza kufanya, bali kuwa na vipaumbele, kujua kipi muhimu zaidi na kuweka rasilimali zako zote kwenye yale muhimu zaidi.
Kuwa na ufanisi mkubwa na uzalishaji wa hali ya juu ni kuchagua machache ambayo ni muhimu zaidi na kuyafanya vizuri kabisa, bila ya kukimbilia kufanya yale yasiyo muhimu.
Kinachowaponza wengi ni kutokutuliza mawazo na nguvu zao sehemu moja. Wanakimbia kimbia na kuhangaika hangaika na mambo mengi, siku inaisha, wamechoka sana lakini hakuna kikubwa ambacho wameweza kukamilisha.
SOMA; Tabia Saba (07) Za Watu Wenye Ufanisi Mkubwa, Na Wanaofanikiwa Sana.
Ondoka kwenye mtego huu, kila unapokuwa na orodha ya vitu vingi vya kufanya, kabla hujaanza kufanya chambua kwanza ni vitu vipi muhimu zaidi kwako wewe kufanya, vile ambavyo wewe tu ndiye unayeweza kufanya na matokeo yake yatakusogeza mbele zaidi.
Uzalishaji na ufanisi ni pale unapoweza kufanya yale muhimu kwa ubora na kuendelea kufanya hivyo tena na tena na tena. Usikimbilie kufanya kila unachoona ni cha kufanya, chambua kulingana na umuhimu wako na fanya yale muhimu tu.
Yasiyo muhimu, yaweke pembeni na utayafanya ukiwa na muda, au wape wengine wanaoweza kufanya wakusaidie kufanya.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,