Hakuna kitu chochote ambacho ukifanya mara moja kitakuwa na manufaa makubwa kwenye biashara yako, hakuna kabisa.

Mteja akinunua mara moja kwenye biashara yako na asinunue tena ni hasara kwako, hakuna faida yoyote unayotengeneza kwa mteja kununua mara moja.

Mteja akija kwako na akanunua kitu kimoja huwezi kutengeneza faida nzuri kwenye biashara yako.

Unapochagua kutekeleza mbinu fulani kwenye biashara yako a ukafanya mara moja pekee hakuna matokeo makubwa utakayoweza kupata kwa kufanyia kazi kitu mara moja.

Faida na mafanikio yoyote unayopata kwenye biashara yako, ni matokeo ya kurudia rudia kufanya chochote inachopanga au kuchagua kufanya kwenye biashara yako.

Kama kuna njia ya kuongeza wateja unaitumia, inabidi uendelee kuitumia mara kwa mara ndiyo uweze kupata matokeo mazuri.

Kama kuna mteja unataka kumuuzia lakini hataki kununua, inabidi uendelee kumkumbusha mara kwa mara mpaka awe tayari kununua. Na wengi hununua baada ya kukumbushwa zaidi ya mara tano.

Biashara ni mchezo wa namba, kadiri namba zinavyokuwa zaidi, za unayofanyia kazi, ndivyo matokeo yanavyokuwa zaidi. Kwa mfano anayetumia njia moja kuwafikia wateja na anayetumia njia tatu, wa njia tatu atawafikia wateja wengi zaidi. Anayeuza mara moja na anayeuza mara tatu, wa mara tatu anatengeneza faida zaidi. Anayefanya kitu mara moja na kuacha na anayefanya mara kumi, wa mara kumi ananufaika zaidi.

Iangalie biashara yako na angalia kila unachofanya sasa, kisha kiongeze zaidi. Na njia bora ya kuongeza, ni kuongeza sifuri. Kama kitu unafanya mara moja, basi ongeza sifuri mbele ya moja na utapata mara kumi. Anza kufanya mara kumi na utaona kama utapata matokeo unayopata sasa.

Kadiri namba zako zinavyoenda juu, kadiri sifuri zako zinavyoongezeka, yaani mara 10, 100. 1000, na hata 1,000,000 ndivyo matokeo ya biashara yako yanavyozidi kuwa makubwa.

Chochote unachofikiria na kufanyia kazi kwenye biashara yako sasa, ongeza sifuri moja na ona ni juhudi kiasi gani utahitaji kuweka ili kufika ngazi hiyo.

Na kuliko ufanye kitu mara moja kwenye biashara yako, bora hata usifanye kabisa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha