Amka mwanamafanikio,
Amka kwenye siki hii mpya, siku bora na siku ya kipekee sana kwa kila mmoja wetu.
Leo ndiyo ile siku ambayo jana ulisema utafanya kesho, hivyo leo huna budi bali kufanya.

Ipokee siku ya leo kwa hamasa kubwa, kwa mipango mikubwa ya kwenda kuchukua hatua ili kupata matokeo bora.

Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari UNAUZIWA NINI?
Kile unachofikiri kwenye akili yako, ni matokeo ya kile ambacho watu wengine wamekuuzia.
Swali ni unafikiria nini muda wote, na umekuwa unauziwa nini na na nani?

Siku moja mtu mmoja aliniambia nikikusikiliza unavyoongea na nikisoma unayoandika napata hamasa kubwa sana, lakini nikilala na kuamka, nakuwa nimerudi kwenye hali ya kukata tamaa.
Na sikushangaa hilo, bali nilimwuliza ni vitu gani anasikiliza kwa wengine.

Kama unakata tamaa kwenye maisha yako, kama unaona mambo hayawezekani, kama unaogopa utashindwa na kama unaona hali inazidi kuwa ngumu, naweza kukubakikishia shida kubwa siyo wewe, shida ni kile ambacho wengine wanakuuzia, kile ambacho umekuwa unasikiliza kwa wengine.

Haijalishi una hamasa kiasi gani, kama utasikiliza kila ambacho kila mtu anasema, kama utafuatilia kila habari, lazima utakata tamaa.

Haijalishi una hamasa kiasi gani, ukienda kwenye vijiwe na hadhithi pekee zinazopigwa pale ni jinsi gani mambo ni magumu, jinsi gani wengi wameshindwa, hutaweza kupiga hatua.

Haijalishi una hamasa kiasi gani, ukianza siku yako kwa kusikiliza kila aina ya habari, kufuatilia kila aina ya mtandao wa kijamii, utauziwa kila jambo baya lililotokea, utaona kila mtu ana maisha mazuri ila wewe tu ndiye unayeteseka, utakata tamaa.

Kuwa makini sana na nini wengine wanakazana kukuuzia, kila mtu ana ajenda zake binafsi.
Na ushauri wangu kwako, ukishachagua ajenda yako, ukishakuwa na hamasa, usisikilize chochote kinachopingana na hamasa uliyonayo.

Na hii ndiyo sababu upaswi kabisa kufuatilia habari, maana nyingi ni hasi na za kukatisha tamaa.
Hupaswi kukaa kwenye mitandao ya kijamii kwa sababu kila ambacho watu wanaonesha kwenye mitandao hiyo siyo maisha yao halisi.
Na hupaswi kabisa, kukaa karibu na mtu yeyote ambaye ameshakata tamaa, mtu yeyote ambaye alishawahi kujaribu kitu akaahindwa, na kaa mbali sana na wale wahubiri wa hali mbaya na itazidi kuwa mbaya.

Hali ni mbaya au nzuri ndani ya kichwa chako, hamasika na chukua hayua kubwa, au wasikilize wakatishaji tamaa na ushindwe hata kuanza.

Ukawe na siku bora sana ya leo rafiki, siku ya kuhamasika na kufanya, siku ya kukaa mbali na wauzaji wa habari za kukatisha tamaa na magumu.
#Fanya #UsinunueKukataTamaa #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYoueLife

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha