Karibu kila mtu anajua kitu gani sahihi kinapaswa kufanyika ili wapate kila wanachotaka.
Ukitaka kudhibitisha hilo, jaribu kuomba ushauri kwa mtu yeyote unayekutana naye, au hata kwenye mitandao ya kijamii, fanya kama vile hujui au umekwama na unahitaji ushauri wa wengine.
Utapata ushauri wa kila aina, kutoka kwa kila mtu. Na wengi watakaokupa ushauri mzuri mno, ukiwaangalia wao wenyewe hawatumii ushauri huo.
Yaani watu watakupa ushauri mzuri ambao ukiufanyia kazi utapata matokeo mazuri sana, lakini wao wenyewe hawautumii ushauri huo.

Labda ni unaomba ushauri kuhusu fedha, hata ambao hawana fedha watakushauri vitu vizuri sana kuhusu fedha, ila wao wenyewe hawajawahi kuvifanyia kazi.
Au unaomba ushauri kwenye mahusiano, kila mtu atakuambia njia sahihi ya kuendesha mahusiano, lakini ukiamua kumfuatilia kila anayekushauri, utakuta wao wenyewe hawafanyii kazi yale wanayokushauri.
Kile ambacho watu wanashauri na kile ambacho wanafanya kwenye maisha yao ni vitu viwili tofauti kabisa.
Na inakuwa ni tofauti kwa sababu kujua na kusema ni rahisi, lakini kufanya ni kugumu.
Kufanya ni kugumu kwa sababu kunahitaji kitu kimoja muhimu sana, ambacho wengi hawana. Kitu hicho ni NIDHAMU.
SOMA; UKURASA WA 1065; Unaweza Kufanya Nini? Maisha Yako Ni Mfano Kwa Lipi?
Unahitaji kuwa na nidhamu ya hali ya juu sana ili uweze kufanyia kazi yale unayojua, uweze kuchukua hatua kwenye yale unayopanga kufanya.
Bila ya nidhamu huwezi kufanya, na chochote unachojua, utajifurahisha kwa kujua lakini hakitakunufaisha sana.
Nimekuwa nasema, kama kila mtu angefanyia kazi ushauri anaotoa kwa wengine, watu wachache sana wangehitaji kupewa ushauri. Lakini wanaohitaji ushauri wamekuwa ni wengi kwa sababu hakuna wanaofanya.
Kwa sababu hata mtu anapoomba ushauri na akapewa, bado kuufanyia kazi ni kugumu. Lakini kama angeona mtu anafanyia kazi, na yeye akaenda kufanyia kazi, isingekuwa ngumu kwake.
Kujua hakutakusaidia chochote kama huna nidhamu ya kukaa chini na kufanya, kuachana na kila kitu na kufanya. Kufanya ndiyo kunaleta matokeo yoyote yale unayotaka. Fanya.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,