Lipo kosa moja kubwa ambalo watu wengi wanafanya na linawazuia sana kupata kile wanachotaka na hata mafanikio kwa ujumla.
Kosa hilo ni kujirahisisha na kutokujithamini kwa namna wanavyopaswa kufanya.
Watu wengi wamekuwa hawajiamini kama kweli wana thamani kubwa, na hivyo wamekuwa wakiogopa kuwataka watu walipe ile thamani ambayo wanaitaka hasa.
Hivyo kwa kuogopa hilo, watu wamekuwa wanajirahisisha sana. Watu wamekuwa hawathubutu kuwaambia watu thamani yao hasa wakiamini kwamba watu hao hawatakubali.

Rafiki yangu, kwenye haya maisha, watu wanakupa kile ambacho unakubali kupokea, kile ambacho unavumilia kupokea. Kama ukiwa mtu wa kukubali vitu vidogo hivyo ndivyo utakavyopata. Ukiwa mtu wa kukubali vitu vikubwa, watu watakupa vitu vikubwa.
SOMA; UKURASA WA 864; Usipunguze Bei, Ongeza Thamani…
Kwenye kila anayekuja kwenye maisha yako, hakikisha anajua ipi thamani halisi wanayoweza kupata kutoka kwako. Na pia wajue gharama halisi wanayopaswa kuingia ili kupata thamani unayotoa.
Usiogope kueleza gharama ya thamani unayotoa, hata kama inaonekana ni kubwa, kikubwa ni kueleza thamani kubwa unayotoa na jinsi inavyoweza kuwasaidia wengine.
Ukikutana na wale wanaosema kwamba gharama zako ni kubwa, usikate tamaa, endelea kuwafikia wale ambao wana uhitaji sana wa kile unachotoa, na siyo muda utakutana na wale ambao wanakithamini kweli na wapo tayari kugharamia.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,