Biashara ndogo ni biashara ngumu sana kufanya, kwa sababu wewe mfanyabiashara ndiyo unakuwa kila kitu kwenye biashara yako. Maamuzi yote kwenye biashara yako yanakutegemea wewe, na kwa wingi wa majukumu yako, ni rahisi kushindwa kuweka mkazo kwenye maeneo muhimu ya ukuaji wa biashara yako. Unapokuwa kwenye biashara ndogo, kila siku kazi yako ni kuzima moto, kushughulika na mambo yanayohitaji kufanyiwa kazi haraka.

Lakini pia biashara ndogo ni nzuri, kwa sababu zinampa mtu ile hali ya umiliki, na kama unawahudumia wateja wako moja kwa moja, basi unaweza kuwapa huduma nzuri, ukawajua vizuri na wao wakakujua vizuri. Ni rahisi kujenga mahusiano bora na wateja wako unapokuwa kwenye biashara yako. Huwa upo usemi kwamba kadiri biashara inavyokuwa kubwa, ndivyo inavyozidi kuwa mbali na wateja wake. Hivyo kwenye biashara ndogo una faida ya kuwa karibu zaidi na wateja.

SOMA; BIASHARA LEO; Mshauri Muhimu Kuhusu Huduma Kwa Wateja Kwenye Biashara Yako Ni Huyu…

Mafanikio kwenye biashara ndogo, yanategemea kitu kimoja pekee, kazi ambayo wewe mfanyabiashara unaweka. Kama tulivyoona, maamuzi yote kwenye biashara yanategemea mfanyabiashara. Hivyo ukomo wa kwanza kwa mfanyabiashara kwenye biashara ndogo ni muda, na ukomo wa pili ni nguvu.

Ili mfanyabiashara mdogo afanikiwe kwenye biashara yake, lazima aelewe ukomo huo alionao na aelewe jinsi ya kuuvuka. Kwa sababu majukumu aliyonayo kwenye biashara yake ni mengi, na mafanikio ya biashara hiyo yanamtegemea sana yeye na kazi anayoweka.

Unapokuwa kwenye biashara yako, unahitaji kufanya kazi kupitiliza, unahitaji kufanya kazi mara mbili ya wanavyofanya wale walioajiriwa. Kwa kifupi, biashara ndogo itakuhitaji mno kuliko kitu kingine kwenye maisha yako. Hivyo lazima ujitoe na ujue unataka nini, la sivyo itakuwa rahisi kwako kukata tamaa na kushindwa.

Kama upo kwenye biashara ndogo, fanya kazi kuwa rafiki yako. Pangilia muda wako na majumu yako vizuri, ili uhakikishe unafanya yale muhimu sana kwa ukuaji wa biashara yako. Kwa sababu zima moto zinapoanza, ni rahisi kusahau yale muhimu na kuhangaika na yale ya haraka.

Huna mbadala wa kuweka kazi kubwa kwenye biashara ndogo, ni uchague kuweka kazi kubwa au uchague kuondoka kwenye biashara hiyo. Hakuna njia ya mkato, hakuna namna ya kurahisisha hilo. Unapokuwa kwenye biashara ndogo, wewe ndiyo biashara na biashara ni wewe, ni vigumu sana kujitenganisha na biashara yako. Na ndiyo maana, unahitaji kufanya kile ambacho kweli unapenda kufanya, unaweza kukifanya muda wako wote.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha