Ili ufanikiwe, unahitaji kushirikiana na wengine, unahitaji msaada na mchango wa watu wengine. Kwa sababu hakuna tunachoweza kupata sisi wenyewe, chochote tunachotaka kinatoka kwa wengine.
Hivyo hitaji muhimu sana kwenye mafanikio yetu ni uwezo mzuri wa kuwasiliana na wengine.
Watu wengi wamekuwa wanakosa kile wanachotaka kwa sababu watu wengine hawajafanya kile ambacho waliwategemea wafanye. Sasa cha kushangaza zaidi, wanakuwa hata hawajawaambia wafanye, ila wanategemea kwamba wao wenyewe watakuwa wanajua na kufanya.
Rafiki yangu, kitu chochote muhimu, unachohitaji wengine wafanya, hakikisha unawaambia wewe mwenyewe na unawaambia kwa njia rahisi ambayo wataielewa. Hata siku moja usijiambie nani asiyejua hili, utashangazwa sana pale utakapojaribu kuuliza, na kugundua wengi sana hawajui.
Hata kama ni jambo dogo kiasi gani, ambalo unahitaji wengine wafanye, wape maelekezo sahihi, na uliza kujua kama wameelewa vizuri.
Kama kila mtu ataweka jitihada kidogo tu kwenye mawasiliano yake na wengine, sehemu kubwa ya matatizo ambayo wengi wanakutana nayo ingeondoka.
Kwa sababu pale watu wanapokutana na matatizo au changamoto, pale watu wanapogombana, kupishana au kushindwa kuelewana, tatizo linakuwa limeanzia kwenye mawasiliano. Kuna mtu ambaye hakueleza vizuri au kuna aliyeelezwa ila hakuelewa vizuri.
SOMA; UKURASA WA 710; Vitu Viwili Muhimu Vitakavyowawezesha Watu Kukuelewa Na Kukuamini…
Chukua muda wako kuwaambia watu vitu vizuri, na kuhakikisha kwamba wameelewa kile ulichowaambia na hatua unazowataka wachukue.
Hii inaanzia kwenye ngazi ya familia, hakikisha kila mtu ndani ya familia anaelewa wapi mnakwenda na kila mtu anapaswa kufanya nini. Kama ni kupunguza gharama, kuongeza ushirikiano na kadhalika.
Inakwenda pia eneo la kazi, kama kuna watu wako chini yako, hakikisha kila mtu anajua majukumu yake. Pia unapotoa maelekezo kwa mtu, yaeleze vizuri kiasi kwamba najua nini anapaswa kufanya.
Kwenye biashara hili ni muhimu mno, kwanza wale wote wanaohusika kwenye biashara yako, kama una wasaidizi, wanahitaji kujua lengo la biashara ni nini, wapi mnakwenda na majukumu yao.
Wateja wako kwenye biashara ndiyo wanahitaji zaidi hili, kwa sababu wateja wa zama hizi hawana taarifa za kutosha lakini wanataka kufanya maamuzi haraka. Hivyo kama kitu hawajakielewa, ni rahisi kwao kukikataa au kuona hakiwafai. Kabla hujajishawishi kwamba uliyempata siyo mteja sahihi, hakikisha kwanza ameelewa kile unachouza na jinsi gani kinaweza kumsaidia.
Rafiki, mawasiliano yako na wengine yanaweza kuchochea mafanikio yako au kuyazuia. Hakikisha unatoa maelekezo sahihi na watu wanaelewa kwa urahisi hatua wanazopaswa kuchukua.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,