Kuna maamuzi mengi ambayo watu huwa wanafanya kwenye biashara zao. Lakini cha kushangaza maamuzi mengi yanayofanywa, ni kwa sababu ya mmiliki wa biashara na siyo kwa sababu ya mteja.

Mtu anaamua kufanya kitu kwa sababu yeye ndiye anayependa kiwe hivyo, na siyo kwamba mteja ndiyo anapenda kiwe hivyo.

Unapokuwa kwenye biashara, jua kabisa bishara siyo yako, bali biashara ni ya wateja. Hivyo maamuzi yoyote unayofanya kwenye biashara yako, lazima yaanzie kwa mteja kwanza.

SOMA; UKURASA WA 817; Usimpe Mteja Majukumu Ambayo Siyo Yake….

Unapotaka kubadili chochote, iwe ni kuongeza au kupunguza kwenye biashara yako, angalia kwanza mteja atanufaikaje, angalia mteja atawezaje kuwa bora zaidi ya alivyokuwa awali. Kama chochote unachofanya hakina manufaa kwa mteja wa biashara yako, hakina umuhimu wa kufanya.

Chochote kipya au unachotaka kubadili kwenye biashara yako, angalia kwanza kinamwathirije mteja wa biashara yako. Angalia mteja ananufaikaje, angalia mteja anakuwaje bora zaidi.

Hata pale unapoingia kwenye biashara kwa mara ya kwanza, unapoanzisha biashara eneo jipya, mfikirie kwanza mteja kabla ya kitu kingine chochote. Maana mteja pekee ndiye atakayeiwezesha biashara iendelee kuwepo.

Mteja ndiye bosi na mwajiri wako kwenye biashara, maamuzi yote ya kibiashara lazima yaanze kwa kumfikiria mteja kwanza kabla ya kitu kingine chochote.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha