Kitu cha kwanza kitakachofanya biashara istawi au kufa ni mauzo. Hili ndilo eneo linaloleta fedha kwenye biashara na fedha ndiyo damu ya biashara. Kama huuzi huna biashara, kama huuzi biashara itakufa.

Mauzo ni eneo muhimu sana kwenye biashara yako, na kama nilivyoeleza kwenye kichwa hapo juu, ndiyo jina la mchezo, yaani ndiyo kitu muhimu sana.

Na vitu vyote muhimu kwenye biashara yako, lazima uweze kuvipima.

Swali ni je unaweza kupima mauzo ya kwenye biashara yako?

Je una wateja wangapi wanaonunua na kwa wastani mteja ananunua mara ngapi na anapokuja ananunua kiasi gani?

Je kadiri siku zinavyokwenda mauzo yakaongezeka au yanapungua?

Kama huwezi kujibu maswali hayo kwa uhakika, haupo makini na biashara yako, kwa hakika hujui unafanya nini na biashara yako na mbaya zaidi hujui hata unaenda wapi na biashara hiyo.

Pima mauzo ya biashara yako, na pima kila siku ili uweze kuchukua hatua muhimu kuongeza mauzo.

SOMA; Njia Tano (05) Za Kuongeza Mauzo Kwenye Biashara Yako Unazoweza Kuanza Kuzitumia Mara Moja Na Kufaidika.

Angalia kila njia unayoweza kutumia kuwafikia wateja wengi zaidi wa biashara yako, angalia namna gani unawashawishi waje kununua kwako mara nyingi zaidi. Na mteja akishafika kwenye biashara yako, hakikisha ananunua kwa kaisi kikubwa zaidi.

Yote hayo yatawezekana kama vitu hivi viwili vitakuwa sahihi;

Cha kwanza lazima uwe na bidhaa au huduma ambayo inatatua tatizo au kutimiza hitaji ambalo watu wanalo. Lazima watu wayaone maisha yao yanakuwa bora zaidi kwa kuwa na bidhaa au huduma unayotoa.

Cha pili lazima uweke kazi na juhudi kubwa kuwafikia wateja sahihi wa bidhaa au huduma unayotoa. Adui wako wa kwanza kwenye biashara ni kutokujulikana. Kama wateja wa biashara yako hawakujui, ni sawa na haupo, maana hawataweza kununua kwako kama hawakujui. Hivyo lazima uweke kazi kubwa na juhudi kuhakikisha wateja wanajua uwepo wako na jinsi unavyowasaidia kwenye maisha yao.

Mauzo ndiyo jina la mchezo kwenye biashara yako, kila siku, kila wakati njoo na mikakati ya kuongeza mauzo zaidi kwenye biashara yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha