Mabadiliko yanatokea pale mimi na wewe tunapochukua hatua ya kufanya vitu kuwa bora zaidi ya vilivyo sasa. Kwa kuchukua hatua, kufanya kitu, kuweka juhudi zaidi, kuweka muda zaidi, kuweka ubunifu zaidi na kuweka umakini zaidi kwenye chochote tunachofanya.

Hakuna mabadiliko ambayo yamewahi kutokana na mabishano, maneno pekee hayabadili chochote, hata kama yangekuwa na ushawishi na usahihi kiasi gani. Ni hatua ambazo watu wanachukua ndiyo zinaleta mabadiliko.

Hivyo rafiki yangu, kuingia kwenye mabishano yoyote, ukifikiri ni jambo sahihi kufanya kwa sababu linaleta mabadiliko, unapoteza muda wako na nguvu zako pia. Ni bora muda na nguvu hizo ungetumia kwenye kufanya vitu, hata kama hutapata matokeo makubwa, angalau utaiona njia.

SOMA; UKURASA WA 876; Kuhusu Kupambana, Kushindana Na Kubishana…

Hata kama unataka kumwelekeza mtu kitu, ambacho ni kinyume kabisa na anavyoamini yeye, utafanikiwa zaidi kama utafanya kwa vitendo. Lakini kwa maneno matupu, mtasumbuana tu. Unaweza kukazana kumshawishi kweli, na kwa ushawishi wako akakubaliana na wewe, lakini ukiondoka atarudi kuamini kile alichokuwa anaamini.

Lakini mtu anapoona, anaamini na kubadilika kwa haraka kuliko kusikia.

Usijihusishe kwenye mabishano kwa mategemeo kwamba utawabadili watu, maneno yana nguvu ndogo sana ya kuwabadili watu, ni vitendo ndiyo vina nguvu kubwa.

Kwenye kila unachotaka kuwashawishi watu, angalia jinsi ya kufanya na siyo kusema pekee. Maneno ni upepo ambao unapita haraka, vitendo vinadumu kwenye fikra za watu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha