Umewahi kupita mahali, ukaona biashara mpya imefunguliwa, ukajiambia siku moja utaenda kununua pale, utakapokuwa na uhitaji. Unapita tena siku nyingine unakuta biashara hiyo ipo, unazidi kuamini suluhisho lako limepatikana. Lakini inatokea siku una uhitaji, unaenda kwenye biashara hiyo na kuambiwa ilishafungwa siku nyingi?

Kila mmoja wetu amewahi kukutana na hali kama hiyo. Na hata kama siyo kwa kuona, basi inawezekana ni kwa njia ya mtandao, unakuwa unauhitaji wa kitu, unatafuta kwenye mtandao, unapelekwa kwenye ukurasa wa watu wanaojitangaza kufanya kitu hicho, wameweka mpaka mawasiliano yao, unachukua mawasiliano na kuwatafuta, lakini wanakujibu hawafanyi tena biashara hiyo.

SOMA; BIASHARA LEO; Jinsi Ya Kuwafikia Wateja Wengi Zaidi.

Watu wengi sana wamekuwa wanaingia kwenye biashara na kuondoka haraka kabla hata wateja hawajawajua vizuri. Mtu anaingia kwenye biashara, akiwa na hamasa kubwa, mwanzoni anakutana na changamoto na anakimbia.

Hupaswi kufanya hivyo kama umechagua maisha ya biashara na ujasiriamali, unapochagua kuingia kwenye biashara ya aina fulani, basi unahitaji kukaa kwenye biashara hiyo kwa muda. Kwa sababu kuna wateja wengi wanajua kuhusu uwepo wako ila hawajapata uhitaji wa kuja kununua. Na wakati mwingine unakuwa hujawashawishi vya kutosha kuhusu kununua.

Hivyo kabla hujafikiria kufunga na kuacha kabisa biashara kwa sababu ya changamoto ulizokutana nazo, hebu anza kuitangaza upya biashara yako, anza kumwambia kila mtu, anza kuwashawishi watu kununua sasa kwa sababu watanufaika zaidi. Fanya hivyo kwa kipindi kifupi na uone kama hutapata matokeo ya tofauti.

Usikimbie kwenye biashara kwa sababu ya changamoto au vikwazo, kila biashara ina changamoto na vikwazo vyake, wapo wateja wengi wanaokujua, wajibu wako ni kuwapa sababu ya kununua sasa ili biashara yako inufaike.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha