Nianze na swali hili muhimu sana, je umewahi kuwashawishi marafiki zako au watu wako wa karibu wakafanya kitu fulani ambacho walikuwa hawajafanya na baadaye wakakushukuru sana?

Labda uliwashawishi kwenda kula kwenye mgahawa fulani, ambao walikuwa na wasiwasi nao, ukawapa uhakika, wakaenda kula na baadaye wakakushukuru sana.

Au labda ni kipindi fulani cha TV ambacho ulikuwa umeona, lakini wao hawajaona, ukawashawishi wakiangalie, wakakiangalia na baadaye wakakushukuru mno kwa kuwaambia kuhusu kipindi hicho.

Inawezekana pia ni kitabu ulichosoma, ambapo marafiki zako walikuwa hawajakisoma, ukawashawishi sana wakisome, wakakisoma kweli na baadaye wakakushukuru sana.

Kama umewahi kuwashawishi watu wakafanya kitu ambacho hawakuwa wamefanya na baadaye wakakushukuru kwa kuwashawishi kufanya hivyo, napenda kukuambia kwamba ndani yako una nguvu kubwa sana ya kuuza.

SOMA; Tabia Tano (5) unazohitaji ili kuwa muuzaji bora.

Njia hiyo hiyo uliyotumia kuwashawishi marafiki zako, ndiyo unayohitaji kutumia kuwashawishi wateja wako. Unawashawishi wateja wanunue unachouza, na baadaye wanakushukuru sana kwa ushawishi wako, maana maisha yao yamekuwa bora.

Kumbuka wakati unawashawishi marafiki zako kufanya kile ambacho hawakuwa wamefanya, ulikuwa unakiamini kweli na unajiamini kweli kwamba watafurahia na kupenda. Hukuwa na wasiwasi wowote juu ya hilo, na ni kujiamini huko ndiyo kuliwasababisha wengi kufanya ulichowaambia.

Hicho pia ndiyo unahitaji kufanya kwenye biashara yako, chochote unachouza, kwanza kiamini sana, kisha jiamini wewe mwenyewe kwenye kuuza. Kisha jua tatizo la mteja ambalo litatatuliwa na amini kabisa ya kwamba kile unachouza kitatatua tatizo hilo.

Ukishakuwa na imani hiyo, sasa nenda kwa wateja wako, wafanye wateja wako waone wanakosa kitu kikubwa sana kwa kutokununua. Na wakishanunua, wafanye wakushukuru sana na kuendelea kununua zaidi.

Kuuza siyo kugumu, kuuza ni sawa na maisha ya kawaida kama utaendesha mauzo kama sehemu ya maisha yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha