Upo usemi kwamba kisichokuua kinakufanya kuwa imara zaidi. Yaani kama umekutana na kitu kibaya kabisa kwenye maisha yako, umekutana na maumivu ambayo ni makubwa sana, lakini hukufa, yaani umeendelea kuwa hai, basi unakuwa imara zaidi baada ya tukio hilo kuliko ulivyokuwa kabla ya tukio hilo.
Hii ni kauli ambayo tunaweza kusema ni kweli kwa baadhi ya watu na siyo kweli kwa wengi. Kwa sababu tukiangalia kwa uhalisia, kuna wachache ambao wamekuwa imara baada ya kupitia magumu. Lakini wapo wengi sana ambao baada ya kupitia magumu, maisha yao yamezidi kuwa hovyo. Hawajafa, lakini maisha wanayoishi baada ya tukio ni mabaya kuliko kabla ya tukio.
Hivyo tunaweza kusema ya kwamba, siyo kinachotokea ndiyo kinafanya maisha ya mtu kuwa bora, bali kile ambacho mtu anafanya baada ya kile kinachotokea. Kwa maneno mengine siyo maumivu ndiyo yanakufanya uwe imara, bali kile unachofanya baada ya maumivu.
SOMA; UKURASA WA 888; Raha Leo, Maumivu Kesho…
Fikra unazokuwa nazo baada ya maumivu, hatua unazochukua baada ya maumivu ndiyo vinavyotengeneza maisha yako baada ya maumivu. Kama utafikiri maumivu hayo ndiyo kikwazo kwenye maisha yako, kama utakata tamaa na kuona hakuna haja ya kuchukua tena hatua, maumivu hayo yatayafanya maisha yako kuwa hovyo zaidi.
Lakini kama utakuwa na fikra kwamba maumivu hayo yamekuja ili kukujenga zaidi, kama utayachukulia kama darasa la kipi muhimu kufanya na kipi siyo sahihi kufanya. Na kama utatumia maumivu hayo kama sababu ya kuchukua hatua zaidi, hutabaki pale ulipo sasa.
Hivyo rafiki, usitegemee maumivu pekee yabadili maisha yako, usitegemee muda pekee ulete mabadiliko kwenye maisha yako, tegemea hatua unazochukua baada ya maumivu na kwenye muda unaofuata maumivu.
Ni unachofanya baada ya maumivu ndiyo kinakufanya uwe imara zaidi au uwe hovyo zaidi. Chagua kuwa imara mara zote, na chochote unachokutana nacho, kama hakijakuua basi kitumie kama kichocheo cha kwenda mbele zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,