Huwa tunasema mafanikio yanaambukizwa.
Kwamba kama utafanya kile ambacho waliofanikiwa wanafanya, basi unakuwa na nafasi kubwa ya wewe kufanikiwa pia.
Na huu ndiyo umuhimu wa kuzijua tabia za watu waliofanikiwa ili kuweza kuziingiza kwenye maisha yetu pia.
Lakini kuna tatizo moja kwenye tabia za watu waliofanikiwa, kadiri unavyozidi kuwafuatilia wengi, unagundua kwamba nyingi katika tabia hizo zinapingana, hivyo usipokuwa makini utashindwa kabisa kuchukua hatua.
Mfano utakuta baadhi ya waliofanikiwa wanaamka asubuhi sana, wakati wengine wanachelewa sana kulala. Utakuta baadhi wanajali sana kuhusu fedha, huku wengine wakiona fedha ni matokeo. Kwenye kila tabia utakayojifunza, utakuta kuna wengine wanafanya kinyume na tabia hiyo na wamefanikiwa sana.
SOMA; TABIA ZA MAFANIKIO; Mambo Muhimu Ya Kuzingatia Wakati Unajenga Tabia Za Mafanikio.
Hivyo basi, unapofika kwenye hatua kama hiyo, unapokuwa njia panda, hujui njia ipi uchukue, ndipo unapohitaji kuwa na msingi sahihi wa kufanya maamuzi.
Kikubwa unachopaswa kujua ni kwamba, huhitaji kuiga kila kitu kwenye maisha ya aliyefanikiwa ili na wewe ufanikiwe. Bali unachopaswa kufanya ni kuchukua yale ambayo yanakusogeza karibu zaidi na malengo yako.
Hivyo basi, lazima kwanza uwe na malengo, lazima uwe na maono, lazima ujue wapi unataka kufika, kabla hujaanza kujifunza tabia za waliofanikiwa. Ukianza na tabia kabla hujajua wapi unaenda, lazima utajikuta njia pana.
Lakini ukishajua wapi unaenda, kila tabia unayojifunza unajiuliza inakusogezaje karibu zaidi na unakoenda. Na hapo unakuwa na hatua za kuchukua na siyo kuwa njia panda.
Usipoteze muda kwenye kuangalia kipi sahihi au kipi siyo sahihi, nani yupo sahihi au nani hayupo sahihi, badala yake tumia muda huo kuchagua kipi utafanyia kazi ili kufikia malengo yako.
Hiyo ndiyo njia pekee tabia za wale waliofanikiwa zitakusaidia sana.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,