Kosa moja ambalo wafanyabiashara wengi wanafanya pale wanapochagua biashara ya kufanya, ni kuangalia wafanyabiashara waliofanikiwa kwenye biashara fulani na kufikiri hiyo ndiyo biashara inayolipa.

Lakini wanapoingia kwenye biashara hiyo, wanagundua siyo rahisi kama walivyoona kwa nje. Wanakutana na changamoto nyingi na hata wateja hawawi rahisi kuuziwa kama walivyofikiri.

Rafiki, ukiona kuna mfanyabiashara anauza sana kwenye biashara fulani anayofanya, jua hauzi kwa sababu ya biashara hiyo, bali anauza kutokana na hamasa hiyo. unaweza kumtoa hapo na ukampeleka kwenye biashara nyingine na akawaweza kuuza vizuri au akashindwa kabisa kuuza.

Kitakachofanya biashara yako ifanikiwe siyo aina ya biashara unayofanya, wala siyo kile unachouza, bali hamasa uliyonayo kwenye kile unachouza.

Kama umehamasika kweli, kama una hamasa isiyopoa juu ya kile unachouza, kama mtu akija kwako hawezi kuondoka bila ya kuwa amehamasika sana, utauza sana.

SOMA; BIASHARA LEO; Kwa Nini Mitandao Ya Kijamii Haina Faida Kubwa Kwako Kibiashara Kama Unavyodhani.

Nafikiri wewe mwenyewe unaweza kuwa shahidi mzuri, hujawahi kwenda kwenye biashara fulani, ukatoka ukiwa na hamasa na ukataka kurudi tena zaidi na zaidi?

Sasa unachohitaji kufanya wewe, ni kuhamasika sana juu ya kile unachouza. Kwanza kukijua kwa undani, kisha kujua kinawasaidiaje wateja wako, halafu unakiamini sana, kiasi kwamba mteja asiponunua basi unamwonea huruma kwa sababu anafanya makosa makubwa kwenye maisha yake.

Sasa unapokutana na mteja, ukiwa na hamasa hiyo kubwa, unahakikisha humwachi mteja wako aondoke hivi hivi bila ya kuwa amehamasika sana. Na ni hamasa mteja anayopata kutoka kwako ndiyo inampeleka kwenye maamuzi ya kununua.

Kumbuka siyo tu kwamba unauza, bali pia unasambaza hamasa. Sasa huwezi kusambaza usichokuwa nacho. Kuwa na hamasa kubwa sana kisha isambaze kwa wateja wako. Wengi sana watanunua.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha