Uhai wa bishara yoyote unatoana na kitu kimoja, mauzo.
Mauzo ndiyo njia pekee ya kuleta fedha kwenye biashara yako.
Hivyo kwenye biashara yako, hakuna kitakachoweza kutokea mpaka pale mteja anapotoa fedha kununua unachouza.
Hivyo nguvu zako zote unapaswa kuziweka kwenye kuhakikisha mteja anaelewa na kuwa tayari kununua.
Lakini pamoja na umuhimu wa mauzo kwenye biashara, imekuwa ndiyo kitu cha mwisho kwenye msisitizo wa wafanyabiashara wengi.
Wengi hupanga kila kitu, hufanya tafiti juu ya tafiti na kuboresha biashara zao watakavyo, lakini wanakosa kujiamini na kumwambia mteja nunua hichi na nina uhakika kitakusaidia sana.
Fanya mauzo kuwa kipaumbele kikuu cha biashara yako, na chochote unachofanya kwenye biashara, jiulize kinachangiaje kuongeza mauzo. Kama hakina mchango kwenye mauzo, hakipaswi kuwa kipaumbele.
Uza, na kila unachofanya kichangie kwenye mauzo.
Na mauzo yako yote yatokane na mahusiano mazuri unayojenga na wateja wako na siyo tu kuuza halafu mteja asitake kurudi tena kwako. Tengeneza mahusiano mazuri na wateja wako na wakuwa wanunuaji wazuri kwako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,