Watu wengi wanapokuwa na biashara ndogo zinazoshindana na biashara kubwa huwa wanajiona kama wapo upande wa kushindwa.
Huwa wanaona biashara kubwa kwa sababu ina rasilimali nyingi basi itawashinda kwa urahisi sana.
Lakini ipo njia ya biashara ndogo kuishinda biashara kubwa, ambayo wala haihitaji gharama za ziada.
Njia hiyo ni kutengeneza mahusiano bora na wateja wako.
Kwenye biashara ndogo, ni rahisi sana kutengeneza mahusiano bora na wateja wako. Ni rahisi kumjua kila mteja na kujua uhitaji wake, pia kumhudumia kulingana na uhitaji wake.
Lakini kwenye biashara kubwa hilo ni gumu, kwa sababu kuna mifumo mingi, mteja anachukuliwa kama sehemu ya takwimu na siyo mtu. Pia mteja anapoenda kwenye biashara kubwa, siyo mara zote anakutana na mtu yule yule ambaye amekuwa anamhudumia. Kuna siku atakutana na mtu anayemhudumia vizuri, siku nyingine mtu akamhudumia vibaya.
Lakini kwenye biashara yako ndogo, unaweza kumhudumia kila mteja vizuri na kila wakati.
Unapokuwa kwenye biashara ndogo inayoshindana na biashara kubwa, usihangaike kushindana kwa vitu vingine kama kupunguza bei au kupiga kelele. Badala yake shindana kwa kutengeneza mahusiano bora na wateja wako. Wafanye wateja waone unawajali zaidi na unawajua kuliko wanavyokwenda kwenye biashara kubwa.
Njia hii siyo rahisi kuikuza pale biashara yako inapokuwa, lakini hata biashara inapokua, hakikisha mahusiano ya biashara na wateja wako yanaendelea kuwa kubwa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,