Kwa kiingereza wanasema out of sight out of mind. Kama hukioni kitu, huwezi kukifikiria. Na pia kinyume chake itakuwa sahihi, kama hufikirii kitu, huwezi kukiona.
Sasa utajiuliza kauli hii ina matumizi gani kwenye biashara yako. Na ukweli ni kwamba, kauli hii ina kila kitu kuhusu wateja wa biashara yako.
Kuna wateja wananunua kwako mara moja au mara chache, kisha huwaoni tena. Unajiuliza wateja hao wameenda wapi?
Huenda walikutana na changamoto fulani ya kimaisha, au walisafiri au mambo mengine yaliwatinga. Lakini baadaye wakarudi vizuri, ila wakawa wameshakusahau kama wewe unauza kitu wanachokihitaji.
Na hapo ukichukulia kwamba ameshakutana na wafanyabiashara wengine, wanaomuuzia kile ulichomuuzia, hawezi hata kukumbuka kama upo.
Hivyo unahitaji kutumia kauli hiyo hapo juu, kuwafanya wateja wako wakufikirie na hata kukuona.
Na njia nzuri ya kufanya hivyo ni kukusanya mawasiliano ya wateja wako, hasa namba zao za simu. Na ukiona mteja hajaja kwenye biashara yako kwa muda, wasiliana naye, fanya kumsalimia na kutaka kujua anaendeleaje.
Utashangaa jinsi wengi watakavyokuwa wamesahau kama upo kwenye biashara yako. Wapo watakaokuuliza hivi bado unauza vitu fulani?
Mawasiliano yako yanakuwa yamewafanya waanze kufikiria kuhusu wewe na wakifikiria kuhusu wewe ni rahisi kuja kukuona na kununua tena kwako.
Ukiwaacha wateja wapotee, bila ya kuwakumbusha na kuwafanya wafikirie kuhusu biashara yako, utaendelea kupoteza wateja wa biashara yako.
Wafanye wateja wako wakufikiria kwa muda mwingi na wataendelea kununua kwako mara kwa mara.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,