Kila mfanyabiashara huwa anapenda kuwa na wateja wengi awezavyo, kwa sababu ni kupitia wateja ndiyo biashara inatengeneza faida.
Hivyo ndoto ya kila mfanyabiashara ni kuwa na wateja wengi zaidi, na wengi wanapoanzisha biashara, huwa wanalenga kumuuzia kila mtu.
Hivyo hutawakuta wakiweka mipango ya kuwafikia wateja wa aina fulani, wao watakuwa wanakazana kumfikia kila mtu.
Ukweli ni kwamba, hakuna biashara ambayo mteja wake ni kila mtu, hivyo kama upo kwenye biashara na unajiambia wateja wako ni kila mtu, hujui biashara unayofanya.
Kwenye biashara hakuna moja kwa ajili ya wote. Hakuna kitu kimoja kinachowafaa wote. Na hata kitu kile kile, watu watajisikia vizuri zaidi kununua kwa mtu fulani kuliko kununua kwa mtu mwingine.
Hivyo wajibu wako mkubwa kama mfanyabiashara ni kuchagua aina ya wateja ambao utawahudumia vizuri mno, kisha kupuuza wengine wote. Unapochagua aina fulani ya wateja, na kuwapa kile wanachotaka, na kuweka nguvu zako zote katika kuhakikisha wanapata huduma bora zaidi, unajiweka kwenye nafasi ya kufanikiwa zaidi kuliko ukikimbizana na kila aina ya mteja.
Kwa sababu unapoanza kukimbizana na kila aina ya mteja, huduma zako zinakuwa chini na wateja hawaridhiki. Pia kuweza kumhudumia kila aina ya mteja unakuwa mzigo mkubwa kwako ambao hutaweza kuutekeleza.
Achana na moja kwa ajili ya wote, badala yake chagua aina ya wateja unaoweza kuwahudumia vizuri na peleka nguvu zako zote kwa wateja hao. Watakuletea wateja wengine kama wao na biashara yako itakua zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,