Unapoanzia biashara yako chini kabisa, watu wengi hawakupi uzito.

Watu wengi wanaona ni biashara ndogo, ambayo haiwezi kufanikiwa.

Wapo mpaka watakaokukatisha tamaa na kukuambia huwezi.

Sasa wewe unakomaa, una ndoto yako unayofanyia kazi na biashara inaanza kukua, biashara inaonesha mafanikio makubwa.

Hapo sasa ndipo hatari ya biashara yako inapoanzia.

Biashara yako inapoanza kukua na kufanikiwa, utaanza kuona kila mtu anakupa ushauri kipi cha kufanya ili ikue zaidi. Utapokea ushauri wa kila aina kutoka kwa kila mtu, ambaye atakuambia kipi ufanye ili kukua zaidi.

Kumbuka wengi walikupuuza ulipokuwa na biashara ndogo, lakini sasa wamekuwa wataalamu wa biashara yako kwa sababu imefanikiwa.

Na nasema hii ni hatari kwa sababu ni kwenye hatua za aina hiyo biashara nyingi sana zimepoteza dira na kufa. Kwanza ule ukuaji unakuwa umemchanganya mfanyabiashara ambaye hakuwa amejipanga kupokea ukuaji, pili wale anaompa ushauri wanazidi kumchanganya zaidi.

Sisemi kwamba biashara yako ikishakua hupaswi kusikiliza ushauri wa wengine, ila ninachosema, ushauri wowote unaopokea usiufanyie kazi kabla kwanza hujapitia maono na ndoto zako kubwa kibiashara, ili kujua wapi unaenda na ushauri huo unakufikishaje pale.

Maamuzi yoyote unayofanya kwenye biashara, usiangalie matokeo ya haraka, bali angalia matokeo ya mbeleni, kulingana na maono unayoyafanyia kazi. Unaweza kusikiliza kila aina ya ushauri, lakini lazima uchambue mwenyewe kuona kipi ukifanyia kazi kinakupeleka kwenye mafanikio ya ndoto yako.

Usiruhusu ukuaji wa biashara yako kuwa hatari ya kifo cha biashara yako. Endelea kusimamia ndoto yako kibiashara na kila siku kazana kuwa bora zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha