Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi nyingine nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari WALIOSHINDWA WANATAKA NA WEWE USHINDWE…
Kuwa makini sana na watu walishindwa na kukata tamaa na maisha yao.
Kwa sababu hawatakuruhusu kabisa wewe ushinde na kufanikiwa.
Kwa sababu wanajua wewe ukishinda, inamaanisha wao ni wazembe au hawajui njia sahihi ya kufanikiwa.

Hivyo utakapoanza safari yako ya mafanikio, watakaokuwa wa kwanza kukutisha na kukukatisha tamaa watakuwa wale ambao walishajaribu na wakashindwa.

Sasa unachopaswa kuelewa, na ili watu hao wasikuyumbishe ni hiki, KUSHINDWA SIYO TATIZO, TATIZO NI KUKATA TAMAA.
Jua kabisa kwa kile wanakuambia watakuwa sahihi, kwamba itakuwa ngumu na kwamba utashindwa.
Waambie ndiyo utashindwa, lakini hutakata tamaa.

Na hivyo ndivyo unavyopaswa kuendesha maisha yako, kutokukata tamaa, hata kama kitu gani kimetokea.
Kama bado upo hai, amka na upambane.
Wale waliokata tamaa watataka na wewe ukate tamaa, watakuwa wanakukumbusha mara kwa mara umuhimu wa kukata tamaa ili uwe kama wao.

Hao ni watu unaopaswa kuwa nao mbali sana, na kuwapuuza kwenye mengi wanayokutisha nayo.
Kwa mfano, unajua kabisa kwamba mafanikio makubwa ni magumu kufikia, njia ina kushindwa kwingi, je unahitaji tena kuendelea kukumbushwa hilo?
Tumia muda na nguvu zako kufanya na siyo kuwasikiliza walioshindwa, wanaohubiri habari za kushindwa.

Uwe na siku bora na ya kipekee sana leo, siku ya kuuendea ushindi bila ya kukata tamaa.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha