Mpendwa rafiki yangu,

Ni bora ni kuambie ukweli kuliko kusema laini na kukubembeleza. Kabla ya watu hawajapata ajira utawasikia wengi kweli wanakuwa na mipango mizuri na wengi wanakuwa na kauli yao moja kuwa ninaingia kwenye ajira kwa ajili ya kutafuta mtaji tu. Na kama nikishapata mtaji tu na kwenda kufungua biashara yangu.

Ukienda kumuuliza mwajiriwa ambaye amekaa kazini zaidi ya miaka kumi na ukamuuliza kwanini huna biashara basi sehemu pekee ambayo atakimbilia kujificha ni kukuambia sina mtaji. Huu ni unafiki mkubwa umekaa zaidi ya miaka 10 katika ajira halafu bado unasema huna mtaji hata ukipewa miaka mia moja kama umeshindwa kujitoa kafara ya kuanzisha biashara hutoweza kuanzisha kwa sababu biashara ni hatari na watu wengi hawapendi kuwa na vitu vinavyowasumbua hivyo wanapenda vitu ambavyo haviwasumbui. Licha ya biashara kuwa ni hatari lakini ndiyo inayolipa na asili ni hivi yule anayekabiliana na hatari ndiyo anaweza kufanikiwa zaidi kuliko yule mtu anayejilinda.

Michango

 

Kama mpaka leo uko kwenye ajira zaidi ya miaka kumi na bado unalalamika huna mtaji jibu rahisi nitakalokupa wewe ni mzembe, na mzembe huwa haishiwi sababu. Hakuna jambo rahisi, watu wanashindwa kujitoa katika maisha yao kupata kile wanachokitaka kwa sababu ya uzembe, tumekuwa na tunajificha katika miamvuli ya sababu ili kuficha uzembe wetu.

Unatakiwa kukua na kuacha sababu za sina mtaji, unataka wahisani watoke nje ndiyo waje kukupa mtaji? Hivi ungekuwa unajilipa asilimia kumi au hata tano ndani ya miaka mitano au hiyo kumi mpaka sasa hivi ungekosa huo mtaji? Huoni kama ni uzembe huo? Unaweza kufanya chochote kama ukiamua kufanya lakini kama hujaamua ni ngumu.

SOMA; Huyu Ndiye Mtu Asiyeishiwa Sababu Katika Maisha Yake.

Watu wengi wanavumilia maisha kwa sababu yale maisha wanayoishi hayajawakera kiasi kwamba wabadilike. Kama kuna hali inakukera haswa huwezi kusubiri kuchukua hatua unaipenda na haikuumizi ndiyo maana unaipenda kuwa nayo.

Hatua ya kuchukua leo, kama uko kwenye ajira na ulisema unaenda kutafuta mtaji ili ufungue biashara na mpaka leo bado unalalamika huna mtaji basi wewe ni mzembe mkubwa. Acha uzembe haraka iwezekanavyo na chukua hatua haraka.

Kwahiyo, usipende kujificha katika sababu ya sina mtaji, ona uchungu na maisha yako , mtu anayejitambua hawezi kila siku kujikimbia kwa sababu kuna watu wanajikimbia kila siku katika maisha yao. Jipende maisha ni yako.

Ukawe na siku bora sana ya leo rafiki yangu.

Rafiki na mwalimu wako,

Deogratius Kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com , kessydeo@mtaalamu.net

Unaweza kutembelea tovuti yangu kwa kujifunza zaidi kila siku na kupata huduma mbalimbali kama vile vitabu, kwa kutembelea tovuti  hii  hapa  www.mtaalamu.net/kessydeo .

Asante sana na karibu sana !