Biashara haina tofauti sana na vita, kwa sababu kufanikiwa kwenye biashara kunakutaka uwe shujaa kama walivyo mashujaa wa vita.

Biashara nyingi zinazoanzishwa huwa zinakufa kwa sababu wanaoanza biashara hizo wanakuwa hawajajiandaa kisaikolojia kupambana na changamoto mbalimbali za biashara.

Wengi hufikiri biashara ni wazo na mtaji, vingine vitakwenda. Lakini biashara ni zaidi ya hapo, kuna mengi watu wanakutana nayo kwenye biashara na wanakuwa hawana maandalizi.

Hivyo kama unahitaji kukumbuka kitu kimoja kuhusu mafanikio ya biashara, basi ni ushujaa. Mafanikio ya biashara yako ni matokeo ya wewe kuwa shujaa.

Kuna hatua mbili za kishujaa ambazo kila mfanyabiashara anapaswa kuzichukua ili biashara yake iweze kufanikiwa.

Hatua ya kwanza; chukua hatua kama vile hakuna kikomo.

Kikomo chochote kwenye maisha na hata kwenye biashara, kinaanzia kwenye akili, kwenye fikra zetu. Unaosema siwezi kufanya hiki au kile, hayo ndiyo matokeo unayopata.

Kwenye biashara yako, chukua hatua kama vile hakuna ukomo wowote kwako kibiashara. Mteja akisema anataka kitu fulani mwambie utakipata, hata kama hujui anakipataje. Unakubali kwanza kisha unaanza kuona ni kwa namna gani unampa mteja kile ambacho anataka. Muhimu ni kile anachotaka mteja kiwe kinaendana na biashara unayofanya.

Usijiwekee ukomo wowote, usiweke mipaka kwamba kipi biashara inaweza kufanya kipi haiwezi. Biashara inapaswa kuchagua tatizo gani la wateja inatatua na isiweke ukomo kwenye kiasi gani cha kutatua.

Hatua ya pili; chukua hatua kama vile hakuna kushindwa.

Hofu ya kushindwa ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo na mafanikio ya wengi. Wengi huwa wanapanga makubwa, lakini wanapofikiria kushindwa, wanaacha kabisa kuchukua hatua.

Kwenye biashara yako unapaswa kuchukua hatua kama vile hakuna kushindwa. Pamoja na kuwa na hofu kwamba mambo yanaweza kwenda vibaya na ukakosa unachotaka, unahitaji kuchukua hatua hivyo hivyo.

Unapochukua hatua kama vile hakuna kushindwa, utashangaa namna utakavyoweza kufanya makubwa na ambayo wengi wanayahofia.

Rafiki, hatua hizo mbili nilizokushirikisha unaona mwenyewe kwamba siyo rahisi, ndiyo maana nikasema ni hatua za kishujaa. Najua kwa akili za kawaida utakuwa na mengi ya kujitetea kwamba kwa nini huhitaji kuchukua hatua hizo, na utakuwa sahihi kabisa.

Lakini kumbuka, kama unataka mafanikio makubwa kwenye biashara unayofanya, basi huna budi kuchukua hatua za kishujaa, ambazo siyo tu zitakuletea mafanikio, bali pia zina hatari ya kuua kabisa biashara yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha