Huwa tunapenda sana kukubalika na kila mtu. Tunapenda watu watukubali kwa vile tulivyo na kwa kile tunachofanya.
Lakini mara nyingi hilo limekuwa halitokei, siyo watu wote wamekuwa wanatukubali kwa vile tulivyo.
Hasa wale ambao tunataka sana watukubali, ndiyo kabisa hawana muda na sisi.
Kutegemea wengine wakukubali ndiyo uweze kufanya kitu, ni kutoa majukumu yako kwa watu wengine.
Hakuna mtu mwenye jukumu la kukukubali wewe ila wewe mwenyewe.
Kujikubali wewe mwenyewe ndiyo jukumu lako kuu kwenye maisha.
Chagua kuishi maisha halisi kwako, maisha yenye maana kwako na ujikubali kwa maisha hayo.
Halafu waache wengine nao waishi maisha yenye maana kwao.
Wale wanaokubaliana na maisha unayoishi, watakuja wenyewe kwako na wala hutakuwa na kazi ya kuwatafuta au kuwashawishi.
Na utakapochagua kuishi hivyo, utashangaa jinsi itakavyokuwa rahisi kwa wale waliosahihi kwako kukufikia.
Lakini unapokazana kuwafanya watu wakubaliane na wewe, unapokazana kumfurahisha kila mtu, unajikuta unachoka na huwapati watu sahihi kwako.
Ni jukumu lako kujikubali wewe mwenyewe na kuchagua kuishi maisha yenye uhalisia kwako binafsi. Wengine watakufuata kulingana na maisha yaliyo sahihi kwao.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,