Wafanyabiashara wavivu na wasiotaka kuweka kazi, huwa wanatumia njia moja kwenye kushindana. Njia hiyo ni kushusha bei na kuuza kwa bei rahisi zaidi ya wengine. Ni njia ambayo kwa haraka inaweza kuongeza wateja na faida, lakini baadaye inakuwa mzingo mkubwa kwa mfanyabiashara.
Hii ni kwa sababu, kila mtu anaweza kupunguza bei, na washindani wako wanapogundua umepunguza bei na kupata wateja wengi, nao atapunguza bei. Kinachotokea ni bei zinaenda chini, faida inakuwa kidogo, huduma zinakuwa mbovu.
Badala ya kukimbilia kupunguza bei, kitu ambacho kila mtu anaweza kufanya, unaweza kwenda kinyume, kwa kufanya kile ambacho wengi hawawezi kufanya.
Unachohitaji kufanya ni kuongeza thamani zaidi unayotoa kwa wateja wako. Mfanye mteja aone kama amekuibia hivi, mfanye aone akilinganisha alichopata na fedha aliyolipa, amepata zaidi.
Na ukishaweka thamani kiasi hicho, hutahangaika na wanaopunguza bei, kwa sababu wateja wanapopata thamani, bei inakuwa siyo kikwazo tena kwao.
Kazana kuweka thamani zaidi, wape wateja kile ambacho hawawezi kukipata kwa wafanyabiashara wengine. Kwa namna hii biashara yako itadumu na kukua zaidi.
Hili linahitaji kuweka kazi zaidi kuliko kupunguza bei, na kama umeingia kwenye biashara kweli, basi usiogope kuweka kazi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,