Kuna vitu vingi sana ambavyo wafanyabiashara wengi huwa wanafanya. Lakini sehemu kubwa ya vitu hivyo ni kupoteza muda na nguvu pia.

Unaweza kuwaona watu wapo ‘bize’ sana, wanakazana kufanya kila kitu, lakini ukifanya tathmini ya yale wanayofanya, unagundua kwamba hayakuwa na umuhimu mkubwa.

Kitu chochote unachofanya kwenye biashara yako, lazima kiwe na sifa hizi tatu;

Sifa ya kwanza ni kukuwezesha kuwafikia wateja zaidi wa biashara yako.

Sifa ya pili ni kuwahudumia wateja zaidi, kuwapa thamani zaidi.

Sifa ya tatu ni kuongeza faida zaidi kwa kuongeza thamani au kupunguza gharama za kuendesha biashara yako.

Kama kuna kitu unafanya kwenye biashara yako, ambacho hakigusi eneo lolote kati ya hayo matatu, unapoteza muda wako na unajisumbua wewe mwenyewe.

Na haijalishi wangapi wanafanya, maana watu wamekuwa wanajihalalishia kupoteza muda wao kwenye biashara kwa sababu wengine pia wanafanya hivyo.

Weka vipaumbele kwenye muda na nguvu zako kwa kukazana na yale mambo yenye matokeo bora kwenye biashara unayofanya. Mengine achana nayo au wape wengine wayafanye.

Jua wateja wa biashara yako wanatokea wapi na weka muda na nguvu kuwafikia wateja zaidi.

Jua thamani ipi unatoa kwa wateja wako na kazana kuiboresha zaidi.

Pia kazana kuongeza faida zaidi kwa kuuza kwa wateja wapya, kuuza zaidi kwa wateja ulionao na hata kutoa thamani zaidi. Pia kupunguza gharama za uendeshaji kutakusaidia kuongeza faida zaidi.

Una ukomo wa muda na nguvu, tumia vitu hivyo vizuri ili uweze kukuza biashara yako zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha