Moja ya vitu vinavyoua biashara nyingi ni mazoea. Watu wanakuwa wameanza biashara na kugundua njia moja ya kufanya biashara zao ambayo inawapa manufaa na kutumia njia hiyo kwa mazoea bila ya kubadili au hata kuwa bora zaidi.
Watu wengine wamekuwa wanashauriwa kwamba njia pekee ya kufanikiwa ni kufanya biashara fulani au kufanya biashara zao kwa njia fulani pekee. Hilo pia siyo sahihi.
Hakuna biashara moja sahihi kwa kila mtu kufanya, kwamba mtu yeyote akiingia kwenye biashara hiyo lazima afanikiwe.
Pia hakuna njia moja sahihi ya kufanya biashara yako kwamba ukitumia hiyo lazima ufanikiwe.
Kila biashara ina njia nyingi bora za kuifanya. Na huwezi kuzijua zote kama hujifunzi na kuboresha biashara yako kila siku.
Kama hujaribu mambo mapya, kama huwezi ubunifu kwenye biashara yako, hutaweza kujua njia bora zaidi zilizopo za kufanya biashara yako.
Kila siku unahitaji kuiangalia biashara yako na kujiuliza kipi naweza kuboresha zaidi. Kila siku unahitaji kuangalia huduma ambazo wateja wako wanapata na kujiuliza ni kwa namna gani unaweza kuboresha zaidi.
Kwa kufanya hivi, utaona nafasi nyingi za kuboresha biashara yako na utaweza kukuza zaidi biashara yako kila siku.
Lakini kama utaendesha biashara yako kwa mazoea, ukijiambia tayari umeshajua siri kuu ya mafanikio, utabaki nyuma na biashara yako itajikuta kwenye wakati mgumu.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,