Watu wengi wanapofikiria kuhusu biashara, cha kwanza wanachofikiria ni fedha.

Wanasema hawajaingia kwenye biashara kwa sababu hawana mtaji.

Wanasema hawawezi kukuza biashara zao kwa sababu hawana fedha za kutosha.

Wanasema biashara zao zinakufa kwa sababu hakuna fedha.

Kufikiria biashara kwa upande wa fedha pekee ni kosa ambalo limewazuia wengi kuanzisha na hata kukuza biashara zao.

Biashara siyo fedha, bali biashara ni watu.

Kama ukiacha kuangalia fedha na ukaanza kuangalia watu, utaziona fursa nyingi sana za kuanzisha na hata kukuza biashara yako, hata kama huna fedha.

Kwa mfano kama ukiwaangalia watu, ukaona changamoto na vikwazo walivyonavyo, unaweza kuja na suluhisho ambalo litawasaidia kisha wao wakawa tayari kukupa fedha. Na wakati mwingine, suluhisho ambalo watu wanalihitaji, halihitaji hata uwe na fedha nyingi. Wakati mwingine unaweza kutumia mahusiano yako na wengine na ukaweza kupata fedha za kuwapa watu kile ambacho wapo tayari kulipia.

Kama utaweka juhudi zako kwenye kuwaangalia watu na kujenga mahusiano bora, nakuhakikishia utaweza kuanzisha na kukuza biashara kubwa utakavyo bila ya kujali una fedha au la.

Biashara ni watu, unapojali zaidi kuhusu watu, unapoboresha mahusiano yako na wengine, unaziona fursa nyingi zaidi za kuwasaidia wengine na wao wakawa tayari kukulipa wewe.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha