Somo moja ambalo kila mfanyabiashara anapaswa kulipata kila siku ni umuhimu wa kujali wateja wa biashara hiyo kwanza.

Wengi wamekuwa wanaona hilo siyo sahihi, hasa kwa enzi hizi ambazo wateja siyo waaminifu.

Enzi ambazo mteja anaweza kuamua kukuhama muda wowote na kwenda kununua kwa mfanyabiashara mwingine.

Lakini hizi ndiyo enzi muhimu sana kujenga mahusiano mazuri sana na wateja wako.

Kwa sababu hakuna sehemu yoyote ambayo mteja anaweza kupata huduma bora kabisa. Kila mtu anaangalia anapata nini na hajali mteja ameridhika au la.

Hivyo kama wewe utachagua kuanza kumwangalia mteja kabla hujaangalia faida kiasi gani unapata, utajiweka mbele zaidi ya wengine.

Wateja watajenga imani na wewe, watakuja kwako wakati wote na watawaleta wengine pia kuja kununua kwako.

Lakini pia lazima ufanye hivi ukijua matokeo unayotengeneza siyo ya haraka bali ya muda mrefu. Lazima ujue unaweza usipate faida kubwa leo wala kesho, lakini siku nyingi zijazo, unachopanda leo kitakulipa sana.

Lazima ujue hilo na kuwa na uvumilivu, la sivyo hutaweza kutengeneza mahusiano bora kabisa na wateja wako.

Kama wateja wako watafanikiwa, kwenye kile kinachowasukuma waje kwako unafikiri wataenda kwa nani mwingine kupata wanachopata kwako? Lazima wataendelea kuja kwako.

Lakini kama wateja watashindwa, hawatarudi tena kwako, watatafuta sehemu nyingine ya kupata kile walichokuwa wanapata kutoka kwako.

Weka mafanikio ya wateja wako mbele ya faida na utavuna faidia kubwa kuliko unayokazana kuvuna pale unapoweka wateja nyuma ya faida.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha