Tunapenda kuambiwa hili kwenye upande wa mafanikio, kwamba kama wengine wamefanikiwa basi na wewe unaweza kufanikiwa. Na tunajiambia kabisa kwani wao waweze wana nini na sisi tushindwe tuna nini.

Ni ukweli usiopingika kwamba kile ambacho wengine wameweza kupata kwenye maisha yao, hata sisi pia tunaweza kukipata iwapo tutaweka juhudi zinazohitajika.

Lakini hili pia lina upande wa pili.

Kwamba yale mabaya yanayotokea kwa wengine, yanaweza kutokea kwetu pia.

Wengine wanapata ajali, na sisi pia tunaweza kupata ajali. Wengine wanapoteza mali zao, na sisi pia tunaweza kupoteza mali zetu.

Huwa tunasahau kuangalia hili na kujifunza kutoka kwa wengine ambao wanapitia magumu, mwishowe tunashindwa kujua mambo gani ya kuepuka na hata tunapokutana na magumu hayo, tunakuwa hatuna maandalizi ya kutosha.

Chochote unachoona kinatokea kwa wengine, jua na kwako kinaweza kutokea pia. Hivyo utanufaika sana kama utajifunza kwa wale ambao tayari vitu fulani vinatokea kwao ambapo bado havijaanza kutokea kwako.

Kwa kufanya hivyo utajifunza kuepuka baadhi ya vitu, na pia utakuwa na maandalizi ya kutosha pale vitu hivyo vinapotokea.

Tunahitaji kuacha kujidanganya kwamba labda sisi tunalindwa kwamba hatuwezi kutokewa na mabaya yanayowatokea wengine. Mabaya yanaweza kutokea kwa kila mtu, muhimu ni mtu kuwa na maandalizi ili yasikutokee kama ajali au usiwe na mshangao yanapotokea.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha