Kuna njia mbili za kuuza chochote unachouza. Njia hizo ni kelele na hadithi.
Kwenye kelele, mtu anapaza sauti kwa njia mbalimbali ili kuwafikia wengi wajue kwamba yupo na anauza nini. Matangazo ya vyombo vya habari, matangazo kwenye mitandao ya kijamii ni moja ya aina za kelele za kutangaza na kujaribu kuuza kwenye biashara yako.
Kwenye hadithi, mtu unatengeneza aina a hadithi ambayo watu wataambiana kuhusiana na kile unachouza. Landa ni kwa namna kinavyoboresha maisha yao, au kwa jinsi kinavyotatua matatizo mbalimbali na hata shuhuda za wale waliotumia na wakanufaika.
Kelele ni rahisi na hazihitaji kazi kubwa, pia matokeo yake yanaweza kuonekana haraka, lakini hayadumu. Na mwisho wa siku watu wanajifunza kuepuka kelele, kwa sababu kila mfanyabiashara anapiga aina hiyo ya kelele. Nunua kwetu, tuna kitu bora, bei ni rahisi na kadhalika.
Hadithi ni ngumu, inahitaji kazi na inahitaji muda mpaka hadithi isambae na kuwafikia wengi. Matokeo yake siyo ya haraka, lakini yanadumu kwa muda mrefu. Watu wanapoielewa hadithi yako kibiashara na kuiishi, inakuwa rahisi kwao kuisambaza. Hadithi inaitofautisha biashara yako na biashara nyingine, maana hakuna biashara mbili zinazoweza kuwa na hadithi ya aina moja.
Mwisho wa siku, hadithi inauza kuliko kelele, hivyo weka muda wako mwingi kwenye kutengeneza hadithi bora na kuwashirikisha wateja wako hadithi hiyo na utatengeneza wateja ambao ni bora na waaminifu.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,