“Failure is not a single, cataclysmic event. You don’t fail overnight. Instead, failure is a few errors in judgment, repeated every day.” —Jim Rohn
Siku mpya,
Siku bora,
Na siku ya kipekee sana kwetu wanamafanikio kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari KUSHINDWA SIYO TUKIO, NI MCHAKATO…
Kushindwa, kama ilivyo kufanikiwa, siyo tukio la mara moja, bali ni mchakato.
Hii ni kusema kwamba, watu wanatengeneza kushindwa, kama ambavyo wengine wanavyotengeneza kufanikiwa.
Hutaamka siku moja na kujikuta kwenye madeni, yaani jana ulilala huna madeni, leo umeamka na madeni. Badala yake utatengeneza madeni yako kidogo kidogo. Leo umekopa hapa, kesho umekopa pale, kesho kutwa unakopa pengine ili kulipa kwa awali. Ukishalipa unakopa tena, na unakuja kustuka miaka baadaye upo kwenye madeni mzito.
Hutaamka siku moja na kujikuta kwenye afya mbovu. Bali utaanza uzembe mdogo mdogo kwenye afya yako mara kwa mara. Unakula vyakula visivyo na afya, hufanyi mazoezi, hulindi afya yako, na kidogo kidogo unashangaa mwili wako unakosa ule uwezo uliokuwa nao mwanzo. Unaenda kupima na kujikuta una magonjwa mengi.
Kadhalika, hutaamka siku moja na ujikute kwenye umasikini mkubwa. Bali utatengeneza mwenyewe mchakato wa kuwa masikini na kubaki kwenye umasikini. Utakuwa mzembe, utatumia kipato chako chote kila unapokipokea, hutaweka akiba wala kuwekeza, na hutaweka juhudi zaidi kwenye kile unachofanya. Utaenda na maiaha hayo ya mazoea mpaka unafika siku na kugundua upo kwenye shimo refu la umasikini.
Unapojikuta eneo ambalo hukutegemea kuwepo, au hutaki kuwepo, jua hujafika hapo kama ajali, badala yale kuna mchakato umekufikisja hapo. Bila kujua na kuvunja mchakato huo, juhudi zako za kuondoka hapo hazitozaa matunda.
Jua mchakato uliokufikisha popote ulipo sasa na uvunje ili kuweza kutengeneza mchakato wa kukupeleka unakotaka kwenda.
Uwe na siku bora sana leo, siku ya kuvunja michakato mibovu na kujenga michakato bora kwa mafanikio yako.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha