Rafiki yangu mpendwa,

Je umewahi kuona kama biashara inakuwa ngumu sana kwako kufanya? Je unaona inakuwa vigumu kwa wateja kukuelewa na kununua kile unachouza? Je wateja wengi wanakuambia watarudi kununua lakini hawarudi tena?

Kama umejibu ndiyo kwenye swali lolote katika maswali hayo hapo juu, basi kwa namna moja au nyingine biashara ni ngumu kwako. Wengi wamekuwa wanafikiri biashara ni ngumu kwao kwa sababu ni ngumu kwa wote, labda hali ya uchumi siyo nzuri au wanunuaji hawapo vizuri.

Lakini huo siyo ukweli, haijalishi hali ya uchumi ni ngumu kiasi gani, wapo wafanyabiashara ambao wanaendelea kuuza vizuri bila shida yoyote. Haijalishi wateja hawana fedha kiasi gani, kuna biashara zinauza zaidi na zaidi. Hivyo tatizo siyo wateja wala uchumi, kama biashara ni ngumu kwako, tatizo ni wewe binafsi.

BIASHARA NDANI YA AJIRA SOFT

Na ipo sababu moja kubwa sana kwa nini biashara inakuwa ngumu sana kwako. Sababu hiyo ni wewe kukosa hamasa kubwa kwenye kile ambacho unakiuza. Kama wewe huna hamasa kubwa kwenye kile unachouza, hutaweza kukiuza kwa wengine, haijalishi unataka kuuza kiasi gani.

Zig Zigler, aliyekuwa mwalimu mzuri sana wa mauzo anasema mauzo ni kuhamisha hamasa. Yaani ili mteja anunue, lazima wewe muuzaji uhamishe hamasa ambayo unayo kwenye kile unachouza na uipeleke kwa mnunuaji.

Hivyo basi, kama hujahamasika sana kwa kile unachouza, hutaweza kuhamisha hamasa kwenda kwa wanunuaji na hivyo hutaweza kuuza kwa viwango vikubwa.

Lazima uhamasike sana kuhusu bidhaa au huduma unayouza. Lazima uamini kwamba ndiyo bidhaa bora sana kwa mteja wako kutumia. Lazima uamini pasi na kuwa na shaka kwamba mteja anafanya makosa makubwa kama ataacha kununua kile unachouza wewe.

Bila ya kufikia imani ya aina hii kwenye kile unachouza, itakuwa vigumu sana kwako kuuza kitu hicho.

SOMA; Sifa Tano (5) Za Biashara Inayoweza Kufikia Mafanikio Makubwa.

Na njia bora ya kuamini kwenye kile unachouza na kuhamasika nacho zaidi, ni kwa wewe kuwa mtumiaji wa kwanza wa kile unachouza. Tumia bidhaa au huduma unayouza, kisha tumia manufaa unayoyapata wewe kama sehemu ya kuuza bidhaa au huduma hiyo. Jitumie wewe mwenyewe kama mfano kwenye mauzo yako. Mweleze mteja jinsi ambavyo maisha yako yamekuwa bora sana kwa kutumia kile ambacho unauza.

Ishi biashara yako, kula biashara yako, pumua biashara yako, kila unachowaza, kinapaswa kuhusiana na biashara yako. Hiki ndiyo kiwango cha imani unapaswa kuwa nacho juu ya biashara yako kama unataka biashara iwe rahisi kwako.

Wafanyabiashara wamekuwa wengi sana zama hizi, kuwaambia tu watu wanunue haitaweza kukutofautisha na wengine. Unahitaji kuwa shabiki namba moja wa biashara yako, unahitaji kuiamini sana biashara yako na unahitaji kuwa mtumiaji mkubwa wa kile unachouza. Ni kiwango hiki cha imani ndiyo kitakupa hamasa ya kuweza kuwashawishi wengine wanunue kile unachouza.

Na kama unauza bidhaa au huduma ambayo wewe mwenyewe huwezi kuitumia, labda ni mwanaume unauza nguo za wanawake, hakikisha kuna mtu wa karibu kwenye maisha yako ambaye anatumia kila unachouza.

Mwisho kabisa, kama unafanya biashara inayoenda kinyume na imani au misimamo yako, ni bora ukaachana kabisa na biashara hiyo. Hata kama unajiambia unachotaka ni fedha pekee, biashara itakuwa ngumu sana kwako. Kwa sababu ni rahisi wateja kuona kwamba huamini kwenye kile unachouza, na wao hawatakuamini kiasi cha kuweza kushawishika kununua kwako.

Hata kama unachotaka ni fedha, jua kabisa watu hawapo tayari kutoa fedha zao kama hawajashawishiwa kuamini kwenye kile wanacholipia. Na huwezi kuwashawishi watu waamini kama wewe mwenyewe huamini.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; http://eepurl.com/dDZHvL

Usomaji