Mbinu zote za kuwashawishi wateja kununua zimeshatumiwa sana kiasi kwamba wateja hawajui waamini kipi kati ya vingi wanavyoambiwa na kila mfanyabiashara.

Sifa zote za bidhaa au huduma ambazo watu wanauza zimeshaelezwa mpaka mteja anakuwa na wasiwasi kama kweli sifa zinazoelezwa zipo.

Lakini kuna kitu kimoja ambacho kinamshawishi kila mteja na hakizoeleki.

Kitu hicho ni kumpa mteja uhakika wa kile unachomuuzia. Na uhakika unaompa ni kwamba chochote unachomuuzia, kama hakitafanya kazi, au kama hakitamfaa basi anaweza kurudisha na akapata kilicho bora zaidi au akarudishiwa fedha yake.

Hii ni njia bora kabisa ya kumpa mteja imani, kwa sababu moja ya vitu vinavyowafanya wateja wasinunue ni hofu ya kupoteza. Pale mteja anapoona kuna uwezekano wa kununua halafu kitu kisimfae, basi atasubiri. Lakini kama utampa uhakika kwamba hata kama kisipofaa basi anaweza kurudisha, anakuwa na uhakika na ananunua.

Sasa wafanyabiashara wengi huwa wanaogopa wakiwapa wateja uhakika wa aina hiyo, kwamba wateja watanunua kitu, watumie na kisha warudishe na kudai fedha zao. Ni kweli hilo linaweza kutokea, na litatokea kwa wachache, ila wengi hawatafanya hivyo. Na wale wachache watakaotumia mwanya huo, unaweza kuwarudishia fedha zao na usiendelee kufanya nao biashara.

Mwisho wa siku unahitaji kufanya biashara na wale wanaoamini kwenye biashara yako, na wanaotaka ikue zaidi ili iwasaidie zaidi. Hivyo mteja mwenye kutaka manufaa yake tu bila kujali ya biashara, siyo mzuri kuwa naye.

Wape wateja wako uhakika wa chochote unachowauzia, na wafanye wajue hawawezi kupoteza fedha pale wanaponunua kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha