Kama ikatokea umeacha kuuza leo, je kuna watu watakaokosa kile unachouza?
Je wapo watu ambao maisha yao yatakwama kwa sababu ya wewe kuacha kuuza kile unachouza?
Kama ikitokea leo umeondoka kabisa kwenye biashara unayofanya, je kuna watu ambao watagundua uwepo wako?
Iwapo ukiondoka hakuna anayegundua hata kama haupo, basi jua bado hujawa na biashara. Upo kwenye uchuuzi ambao kila mtu anaweza kufanya na hiyo ni hatari kubwa sana kwako.
Biashara yako inapaswa kuwa sehemu ya maisha ya wateja wako, kiasi kwamba kama hutakuwepo kwa siku moja, watagundua haupo na watakuwa tayari kukusubiri, kwa sababu kuna kitu wanakipata kwako tu na siyo kwa wengine.
Na kitu hicho siyo bei ndogo, bali huduma bora sana kulingana na mahitaji yao.
Daladala moja ikikuacha, utapanda nyingine inayokuja na utafika unakokwenda. Sasa biashara yako haipaswi kuwa ya kubadilishwa haraka pale mteja anapokukosa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,