“The price of anything is the amount of life you exchange for it.” — Henry David Thoreau
AMKA mwanamafanikio,
Amka kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo,
Amka uende kuianza siku hii kwa hamasa na msukumo mkubwa wa kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari GHARAMA YA KITU NI MAISHA YAKO…
Mara nyingi huwa tunakuwa warahisi kusema ndiyo kwa vitu ambavyo haviendani kabisa na sisi kusema ndiyo.
Tunasema ndiyo tukihofia kusema hapana tutakosa kitu fulani.
Kitu ambacho wengi hawajui wakati wanasema ndiyo ni gharama halisi ya kitu.
Gharama halisi ya kitu chochote unachofanya au kukubali ni maisha yako.
Kwa kuwa kufanya chochote na muda wako, ni kuuondoa kwenye mambo mengine muhimu zaidi kwako.
Hivyo unabadilishana maisha yako na kila unachosema ndiyo.
Kwa maneno mengine, kwa kila unachosema ndiyo, unayapoteza maisha yako.
Sasa swali ni je, kila unachosema ndiyo kinastahili kuiba maisha yako?
Je inastahili kuyapoteza maisha yako kwenye vitu ambavyo havina maana yoyote kwako?
Upoteze masaa yako ya siku kufuatilia habari, udaku, maisha ya wengine, kubishana mambo hasiyo na tija?
Anza kupima kila unachofanya au kusema ndiyo kwa kipimo cha maisha yako.
Angalia ni kiasi gani cha maisha unapoteza kwa kila ndiyo unayosema.
Na kama kitu hakistahili kupoteza maisha yako, sema hapana.
Maiaha yenyewe uliyonayo hapa duniani ni hayo uliyonayo, hutapata ya ziada. Usipoteze maisha yako yenye thamani kubwa kwa mambo yasiyo na thamani kwako.
Mambo yenye thamani kwako ni yale yanayochangia kufikia kusudi la maisha yako, mengine ni kelele na usumbufu kwako.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuyalinda maisha yako na kutokuyapoteza kwa mambo yasiyo muhimu.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha