Kama umewahi kuona mti mkubwa kabisa, mti ambao umekuwa unauona kwa ukubwa huo huo miaka yote, ni rahisi kujiambia mti huo haukui. Lakini ukiangalia mtu huo kwa makini, utagundua kula mwaka kuna unene au urefu ambao unaongezeka, hata kama ni mdogo kiasi gani. Pia utagundua kila msimu kuna majani mapya yanazalishwa kwenye mti huo.

Sheria ya asili ni kwamba ukuaji hauna ukomo, kila kitu kinaendelea kukua mpaka pale kinapokufa. Na hii ina maana kwamba, kama kitu hakikui, maana yake kinakufa.

Na hii ni kweli kwenye maisha yetu ya kawaida, kama hukui basi unakufa, kama huendi mbele basi unarudi nyuma. Kwenye maisha hakuna kusimama, ni kwenda mbele au kurudi nyuma, huwezi kusema umebaki pale pale.

Chochote ambacho hakikui kwenye maisha yako kinakufa, na kadiri kinavyokufa ndivyo kitakavyokuletea changamoto kubwa zaidi.

Kama wewe binafsi hukui zaidi, kimaarifa, kihekima na hata kiutu binafsi, basi unakufa, na maisha yatakuwa magumu sana kwako kila siku.

Kama kazi yako haikui, kila siku itakuwa changamoto, utaichoka na hutaweza kupiga hatua.

Kama biashara yako haikui inakufa, na hutadumu kwenye biashara hiyo kwa muda mrefu.

Kama mahusiano yako hayakui yanakufa, na kila siku utakuwa na changamoto kwenye mahusiano hayo.

Kama kipato chako hakikui, hata kama una akiba kiasi gani, hutajisikia vizuri kadiri unavyokwenda, maana utakachokuwa unaona kila unapoangalia kipato chako ni kwamba kinapungia. Na hivyo kama hakuna kipato kipya kinachokuja, utaanza kupata hofu vipi kama kipato chote kitaisha.

Kusudi kuu la maisha ni ukuaji, na ukuaji hauna ukomo mpaka pale kitu au mtu unapofikia kifo chako.

Hivyo kila siku kazana kuwa bora zaidi, kila siku jifunze kitu kipya, kila siku kuza zaidi biashara na kazi yako, kila siku ongeza zaidi kipato chako na kila siku boresha zaidi mahusiano yako.

Ukuaji, hata kama ni mdogo kiasi gani ndiyo unayapa maisha yao maana na hamasa ya kuendelea kuweka juhudi kubwa zaidi na kupiga hatua zaidi.

Usikubali siku iishe bila ya wewe kukua zaidi, kwa sababu utakuwa umechagua kufa, kitu ambacho kitatengeneza matatizo mengi kwenye maisha yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha