Umewahi kwenda kwenye biashara mbili ambazo zinafanana, ukakuta kwenye biashara moja watu wamejipanga mstari kusubiri huduma, wakati biashara nyingine haina mteja kabisa? Yaani watu wapo radhi kusubiri wapate huduma kwenye biashara wanayotaka, kuliko kwenda kupata huduma pengine ambapo wangeokoa muda zaidi.

Waswahili watakuambia anayejaza wateja anatumia dawa, au ushirikina, au kuna namna anafanya kuwahadaa wateja.

Ukweli ni kwamba, wale wanaojaza wateja, wanakuwa wametengeneza upendeleo fulani kwenye biashara zao, yaani wanajiweka kwenye nafasi ambayo wateja wanakuja zaidi kwao kuliko kwenda kwa wengine.

Uzuri ni kwamba, hata wewe unaweza kutengeneza upendeleo kwenye biashara yako, unaweza kuwafanya wateja wachague kuja kwako na waache kwenda kwa wafanyabiashara wengine.

Unachohitaji kufanya ni kujali zaidi ya wengine. Wajali wateja wako zaidi, nenda hatua ya ziada kwa kuwapa huduma ambayo hawajawahi kupata kwa wengine. Yajua matatizo na mahitaji yao kwa undani, na hakikisha kile unachowauzia kinawasaidia kweli kwenye matatizo na changamoto zao.

Ahidi makubwa na tekeleza makubwa zaidi ya uliyoahidi. Na huhitaji kufanya mambo yasiyowezekana, badala yake unahitaji kuwajali zaidi wateja wa biashara yako, kwa kiasi kwamba mteja anajiona yupo kwenye mikono salama wanapokuja kwenye biashara yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha