Kwenye maisha, kitu ambacho ni rahisi kufanya, pia ni rahisi kutokufanya.

Pia kitu ambacho ni rahisi kufanya, huwa hakina thamani kubwa, huwa hakilipi kama mtu anavyoweza kuwa anataka.

Hivyo kwa kifupi, tunaweza kusema kuchagua kufanya vitu rahisi, ni kujiweka kwenye mstari wa kushindwa.

Njia rahisi ya kuingia kwenye biashara ni kuuza vitu vya kawaida, kwa watu wa kawaida, kitu ambacho kila mtu anaweza kufanya, na hivyo kinakosa thamani kubwa.

Na kibaya zaidi ya kuuza vitu vya kawaida kwa watu wa kawaida, ni kushindana kwenye bei, kupunguza bei ili kuwavutia watu wa kawaida waje kwenye biashara yako. Unazidi kujipa kazi kubwa kwa faida kidogo.

Badala ya kujitesa na kuuza vitu vya kawaida kwa watu wa kawaida ni kuchagua wateja wachache, ambao wanajali kile cha kipekee unachotoa, ambacho ni tofauti na maalumu kwa ajili yao.

Toa kitu ambacho wateja wako wanaweza kukipata kwako pekee, kwa sababu wewe unajali zaidi, kwa sababu una mchango wa kipekee unaoweza kutoa kwenye maisha ya wengine.

Biashara siyo kuuza na kununua pekee, biashara siyo kuangalia faida pekee, biashara ni kujitoa kuwahudumia watu wenye shida au uhitaji, kwa bidhaa au huduma unayojua itawasaidia kweli na kujenga mahusiano bora na watu hao kiasi cha wao kukuchukulia wewe kama sehemu ya maisha yao.

Achana na kuuza vitu vya kawaida kwa watu wa kawaida, lenga watu unaoweza kuwahudumia vizuri na hutakuwa na wakati mgumu kwenye kuendesha biashara yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha