Watu wengi wanapoanza biashara, wanaona ukuaji wa kipato, ambao unawaridhisha sana na kuwapa hamasa ya kuweka juhudi zaidi.

Wanaweka juhudi na kipato kinaongezeka zaidi, wanazidi kufurahi na kupata hamasa pia.

Wanaongeza tena juhudi na muda wa kazi, na kipato kinaongezeka. Hapo wanajifunza kwamba ukiongeza juhudi na muda, basi kipato kinaongezeka.

Hivyo sasa wanaanza kuongeza juhudi na muda, na kipato kinafika kwenye kilele. Kila wanapoongeza juhudi na muda zaidi, kipato hakiongezeki. Wanaongeza tena juhudi na muda zaidi, kipato hakiongezeki kabisa.

Kipato kinakuwa kimefikia ukomo, na haiwezekani tena kukiongeza kwa juhudi binafsi na muda na nguvu binafsi. Kwa sababu biashara inakuwa imefikia hatua ambayo juhudi za mtu mmoja zimefika kwenye ukomo.

Njia pekee ya kuondoka kwenye mkwamo huo, njia ya kuondoa kikomo hicho, ni wewe kuacha kuwa biashara yako, wewe kutengeneza mfumo utakaoweza kuendesha biashara yako, bila ya wewe kuwepo kabisa.

Hapa ndipo unapohitaji kuwa na watu wanaokusaidia kwenye biashara yako. hapa ndipo unapohitaji kutumia juhudi, nguvu na muda wa watu wengine. Hapa ndipo unapohitaji kuwa na mfumo wa kibiashara, ambapo biashara inaweza kujiendesha yenyewe bila ya kukutegemea wewe moja kwa moja.

Ili kutengeneza mfumo huo, kwanza lazima uwe na watu wa kukusaidia. Pili lazima kila kinachofanyika kwenye biashara kiandikwe kwa jinsi kinavyofanyika, na kisha mtu apewe kama jukumu lake ambalo anapaswa kulikamilisha na iwepo njia ya kuweza kumpima kama amekamilisha au la, na amekamilisha kwa kiwango gani.

Pale unapoendesha biashara yako kwa kila kitu kuwa kwenye akili yako na kufanya kila kitu mwenyewe, itakuwa rahisi kwako kuendesha biashara, lakini kutakuja na gharama ya ukomo. Unapotengeneza mifumo na kuajiri wengine, utahitaji kupangilia kila jukumu na pia kuwatengeneza vizuri wale unaowaajiri, kitu ambacho kitakuwa kigumu kwako mwanzoni, lakini baadaye kitakupa uhuru wako wa kibiashara.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha