Kama umechagua kuingia kwenye biashara, basi biashara yoyote unayochagua kufanya, angalia miaka mingi ijayo. Angalia miaka mitano ijayo, miaka kumi ijayo na hata miaka 50 ijayo. Je biashara hiyo itakuwepo na je itakuwa imekua zaidi kuliko sasa?
Nakuambia hivi kwa sababu kuna uwekezaji mkubwa utakaouweka mwanzo wa biashara yako, uwekezaji ambao hautakulipa kwa kiwango kikubwa. Lakini baada ya muda utaanza kukulipa sana.
Kila kitu mwanzoni kinahitaji juhudi zaidi, muda zaidi na kazi zaidi. Na wakati huo wa mwanzoni, faida inakuwa kidogo sana. Lakini kadiri unavyoendelea na kitu, unajifunza na kuelewa mambo mengi ya ndani na unajulikana na wengine pia. Unafika wakati ambapo juhudi hazihitajiki kubwa sana, lakini matokeo yanakuwa makubwa.
Hakuna ubaya wowote kwenye kufanya biashara za msimu au za fasheni, bali kama unaangalia mbali, kama una maono makubwa, jenga biashara ambayo inadumu kwa muda mrefu, weka nguvu zako kubwa mwanzoni, tengeneza misingi imara na baadaye utanufaika sana na uwekezaji unaofanya mwanzoni.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,