Kama kila biashara ingeweka rasilimali zake kwenye kuwahudumia vizuri wateja wake, biashara zingefanikiwa sana.

Lakini biashara nyingi zimekuwa zinatafuta njia za mkato za kupata wateja, na moja ya njia hizo ni kuwaangusha washindani wao wa kibiashara.

Kama una washindani wa kibiashara, jambo jema kabisa unaloweza kufanya kwa ajili yako ni kuhangaika na biashara yako na kuhakikisha wateja wako wanapata huduma bora sana.

Usipoteze muda wako kuwasema wabaya washindani wako, wala kutaka kuwahujumu. Mteja wako hajali sana nani anaweza kumshinda mwenzake, yeye anachotaka ni kupata huduma bora, na ataenda kule anakohudumiwa vizuri.

Weka nguvu zako eneo sahihi la biashara yako, kwa kuchagua aina ya wateja utakaowahudumia kupitia biashara yako na wahudumie vizuri sana kiasi kwamba hawatataka kwenda sehemu nyingine.

Mteja siyo kama amekaa akiangalia mnapigana halafu akajiambia naenda kwa yule aliyeshinda. Mteja ana shida, ana uhitaji na anataka kupata anachotaka kwa namna itakayomfaa yeye. Hilo ndiyo jukumu lako kuu kibiashara, kumpa mteja kile anachohitaji kwa namna ambayo ni bora kabisa kwake.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha