Unapaswa kuifanya biashara yako vizuri sana leo,

Na wakati huo huo kujiandaa na mabadiliko yanayoendelea kutokea kwenye biashara yako.

Kwa sababu biashara unayofanya leo, siyo biashara utakayofanya kesho, mwaka ujao, miaka 5 ijayo na hata miaka 10 ijayo.

Mambo yanabadilika, watu wanabadilika na mahitaji yao yanabadilika pia.

Watu wanataka vitu kwa uharaka zaidi, ambavyo ni bora zaidi na kwa gharama ambazo wanazimudu. Watu wanataka kile wanachotaka na kwa ubora wa hali ya juu.

Biashara ambayo haijiandai na mabadiliko, ni biashara ambayo imechagua kufa yenyewe kidogo kidogo, kwa sababu mabadiliko hayakwepeki.

Tunapenda kufanya mambo kwa mazoea, lakini hilo hupaswi kufanya kwenye biashara.

Kama umeichoka biashara, ni bora uachane nayo haraka kuliko kuifanya kwa mazoea. Kwa sababu utatumia muda mrefu kuiua biashara hiyo na utateseka sana kwenye kipindi hicho.

Kila siku fikiria njia bora zaidi za kuifanya biashara yako, njia bora za kuwahudumia wateja wako, njia bora za kuyafanya maisha ya wateja wako kuwa bora zaidi.

Na kila siku unayoanza biashara yako, jiulize kipi unafanya tofauti leo na ulivyofanya jana. Kipi utafanya kwa ubora zaidi, kipi utaanza kufanya na kipi utaacha kufanya.

Kifo cha biashara kinaanza pale leo unapofanya kama jana, na kesho ukafanya kama leo. Hakuna mabadiliko na unakaribisha changamoto kubwa zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha