Wafanyabiashara wengi huwa wanafurahi sana pale wanapokuwa na wateja wengi. Kwa sababu wanaamini wingi wa wateja ndiyo mafanikio ya biashara.

Na huwa hawaelewi pale wanapokuwa na wateja wengi lakini biashara inakufa, hapo ndipo wanaamini kwamba kuna chuma ulete. Haiwezekani wauze kwa wateja wengi halafu biashara isipate faida.

Ipo kampuni moja iliyowahi kuwashangaza sana watu. Kampuni hiyo iliwafukuza wateja zaidi ya elfu kumi kwa wakati mmoja. Wateja hao waliambiwa kwamba kampuni hiyo haiwezi kuendelea kuwahudumia hivyo watafute mahali pengine pa kupata huduma walizokuwa wanapata.

Kilichopelekea kampuni hiyo kuchukua hatua hizo, ilikuwa ni kipimo walichofanya kwa wateja wao. Waliangalia kila mteja, manunuzi anayofanya, faida anayoingizia kampuni na uhitaji anaotaka kwenye kampuni.

Sasa kwenye kundi hilo lililofukuzwa, kampuni iligundua ni wateja ambao wananunua mara chache sana na faida wanayoingizia biashara ni ndogo mno. Sasa kama hiyo haitoshi, wateja hao hao ndiyo waliokuwa wakipiga simu kwenye kitengo cha huduma kwa wateja wakitaka msaada zaidi. Na walipima wakagundua wateja hao, walikuwa wanapiga simu mara kumi zaidi ya wanavyopiga wateja wa kawaida.

Kampuni ilisema hao ni wateja wenye gharama kubwa kuliko faida, hivyo wakaamua kuwaruhusu waende sehemu nyingine.

Rafiki, siyo wingi wa wateja unaoleta mafanikio kwenye biashara yako, bali ubora wa wateja hao.

Kama utaitangaza biashara yako sana, mtu akaja akanunua mara moja lakini asirudi tena, hata kama wamekuja wengi kiasi gani, hiyo ni hasara kwako.

Kama unakuwa na wateja wengi, lakini siyo wanunuaji wa mara kwa mara na hata wakinunua wanataka muda wako wote uutumie kwao hao siyo  wateja wazuri kwako.

Hata kama hujafikia uwezo wa kufukuza wateja, basi kazana kutengeneza wateja ambao wana manufaa kwa biashara yako kulingana na juhudi unazoweka. Wateja ambao wanaielewa biashara yako, wanajua nini wanataka, wanapata nini kutoka kwako na wanakuwa tayari kulipia ili wapate.

Lakini kukimbizana na wateja wanaotaka punguzo, na hata baada ya kuwapa punguzo wanataka ufanye kila wanachotaka wao, ni njia ya uhakika ya kushindwa kwenye biashara.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha