Kitu kimoja ambacho kinapelekea baadhi ya biashara zinazoanza vizuri na kukua kisha zinaanguka vibaya, ni wafanyabiashara kushindwa kusema hapana kwa fursa nzuri zinazojitokeza mbele yao.

Iko hivi, unaanza biashara ukiwa na maono fulani kwenye akili yako. Unataka biashara yako iwe ya aina fulani, iwasaidie watu wa aina fulani na ikupe wewe ule uhuru ambao ulikuwa unataka.

Mwanzoni hakuna anayehangaika na wewe sana, kwa sababu wengi wanaamini biashara hiyo haitadumu sana, ukiachilia tu kufanikiwa. Hivyo unajikuta una uhuru mkubwa wa kuendesha biashara yako kulingana na maono uliyonayo.

Kwa kuendesha biashara yako kwa uhuru huo, inakuwezesha biashara yako kukua sana. Na hapo ndipo watu wataanza kukuona, wataona biashara yako ina uwezo na nafasi kubwa sana ya kukua zaidi.

Na hapo ndipo fursa zinapoanza kumwagika, kila mtu anakuletea fursa ambayo inaonekana ni nzuri sana kwako, na wengine watakuambia unakosa fedha nyingi kwa sababu hufanyi hivi au vile.

Hayo yote wanayokuambia hufanyi siyo kwamba huyajui, bali hayachangii kufikia ndoto na maono uliyonayo. Watu wanaokuja kwako na fursa kubwa na nzuri, wanakushawishi ubadili namna ulivyokuwa unaendesha biashara yako na uendeshe kama wanavyosema wao ili kuweza kunufaika na fursa walizokuja nazo.

Na hapo ndipo biashara inapoanza safari ya anguko. Japo mwanzoni biashara itaonekana kufanya vizuri, baada ya muda biashara itaanza kuyumba na hata kufa. Na kama fursa ambazo mfanyabiashara anazipokea ni nyingi, ndivyo biashara inavyokufa haraka pia.

Sisemi usipokee kabisa fursa mpya kwenye biashara, bali hakikisha fursa unayopokea inaendana na maono yako makubwa. Kama haiendani, usijisikie vibaya kusema hapana, hata kama kuna fedha utazikosa. Usiwe na tamaa ya kupata fedha za haraka huku ukiharibu biashara yako ya baadaye.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha