Ipo zawadi moja kubwa sana unayoweza kumpa kila mtu kwenye maisha yako na akaifurahia sana. Kuanzia kujipa wewe binafsi, kuwapa watu wako wa karibu, kuwapa wateja wa biashara yako na hata kumpatia mwajiri wako. Kwa kuwapa watu zawadi hiyo moja, wanaweza kushirikiana na wewe vizuri na hilo likakuwezesha wewe kupata unachotaka.

Zawadi hiyo muhimu ni kuwa wewe, kuwapa watu wewe kwa uhalisia wako.

Tatizo kubwa tunalokutana nalo kwenye maisha ya sasa ni karibu kila mtu anaigiza. Na maigizo haya hayajawahi kuwa na manufaa ya muda mrefu kwa yeyote.

Watu wanaigiza wakati wa mahusiano, ili waonekane wapo aina fulani au wana vitu fulani. Wanawashawishi wenzao kwa maigizo yao, wanaingia kwenye mahusiano ya kudumu yaani ndoa, maigizo yanakoma na matatizo yanaanza kuibuka, ambayo yanawasumbua kwa kipindi chote.

Mtu anataka kazi, hivyo anaigiza ili kupata kazi hiyo, anadanganya juu ya vitu anavyoweza kufanya, anadanganya ni vitu gani anajali, anaandika wasifu uliojaa maigizo, akieleza vitu anavyopenda na alivyowahi kufanya huko nyuma. Anawashawishi wanaoajiri na wanamwajiri, siku chache baada ya kuanza kazi, maigizo yanakoma na uhalisia wa mtu unaanza kuonekana. Na hapo ndipo matatizo kwenye kazi hiyo yanapoanzia na yanamsumbua mtu kwa kipindi chote.

Kadhalika kwenye biashara, watu wanapotaka kuuza kwa haraka na kupata faida, wanaigiza. Wanatoa madai ambayo siyo ya kweli juu ya kile wanachouza, wanaahidi watu vitu ambavyo siyo sahihi, wanapunguza hata bei ili tu wauze. Lakini baada ya kumuuzia mteja mara moja, mteja hawezi kurudi tena kwa sababu anakwenda kugundua kwamba alidanganywa.

Zawadi pekee unayoweza kuitoa kwa mtu yeyote na ikawa na manufaa kwake na kwako pia, ni kuwa wewe, kuishi uhalisia wako, kuacha kuigiza na kamwe kutokudanganya.

Unapokuwa wewe, watu wanajifunza kuenda na wewe jinsi ulivyo, watu wanajua nini wanaweza kupata kwako na nini hawawezi kupata kutoka kwako. Watu wanajua kipi wategemee kwako na kipi wasitegemee.

Kwa kuchagua kuwa wewe kuna watu ambao utawapoteza, tena wengi, lakini hilo halipaswi kukutisha kwa sababu ungewapoteza tu, hata kama ungewadanganya na ukawapata, bado baadaye ungewapoteza. Hivyo ni bora kuwapoteza mapema kabla hamjaingia kwenye matatizo zaidi.

Kwa kuchagua kuwa wewe unawavutia wale watu ambao ni sahihi kwako, wanaweza wakawa wachache sana, lakini hao ndiyo wenye manufaa kwako na wewe una manufaa kwao. Hivyo ukiwatumia vizuri hao wachache, utaweza kuwapata wengi zaidi wanaoendana na wewe.

Katika watu zaidi ya bilioni saba waliopo hapa duniani, hakuna aliye kama wewe, hivyo chochote unachochagua kufanya kwenye maisha yako, hata kama kila mtu anafanya, kifanye kama wewe na wafanye watu waje kwako siyo tu kwa sababu ya unachofanya, ila pia kwa sababu yako wewe, kwa sababu wanataka kuwa na wewe.

Ishi uhalisia wako, jijengee tabia bora na ziishi hizo, tumia uwezo mkubwa uliopo ndani yako, tumia vipaji ambavyo unavyo, fanyia kazi yale ambayo unayajali zaidi na ongeza thamani kwenye kila unachokigusa.

Uzuri ni kwamba hakuna ushindani kwenye kuwa wewe, kwa sababu hakuna anayeweza kuwa wewe. Na wewe pia usikazane kuwa wengine, maana hutaweza kuwashinda wengine kwa kukazana kuwa wao. Ushindi pekee ulionao ni kwenye kuwa wewe, kuwa wewe na uweze kufanya makubwa kwenye maisha yako na yale ya wanaokuzunguka.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha