Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari NGUVU NI ILE ILE…
Nguvu unayohitaji kutumia ili kufanikiwa, na unayohitaji kutumia ili usifanikiwe ni ile ile.
Unaweza kutumia nguvu hiyo kuweka kazi ili ufanikiwe, au ukatumia nguvu hiyo hiyo kutengeneza sababu kwa nini hufanikiwi.

Unaweza kutumia nguvu hiyo kuishi maisha yenye uhalisia kwako, au ukatumia nguvu hiyo hiyo kuishi maisha ya maigizo.
Unaweza kutumia nguvu hiyo kufuatilia mambo yako na kuchukua hatua kubwa, au ukatumia nguvu hiyo kufuatilia maisha ya wengine na usichukue hatua yoyote kubwa.

Unaweza kutumia nguvu hiyo kuwa mwaminifu na kufanya yale ambayo siyo sahihi, au ukatumia nguvu hiyo kufanya yasiyo sahihi na kuyaficha ili wengine wasijue.
Unaweza kutumia nguvu hiyo kujifunza kwa kujisomea vitabu na maarifa mengine muhimu kwa mafanikio, au ukatumia nguvu hiyo kufuatilia habari za udaku na kuperuzi mitandao ya kijamii ambayo hakuna kikubwa unachojifunza.

Rafiki, ili kufanikiwa zaidi, huhitaji kupata nguvu ya ziada, bali unahitaji kubadili matumizi ya nguvu zako uliyonayo kwa sasa.
Kwa sababu ni nguvu hiyo hiyo unayoitumia sasa kwenye mambo mengine, ndiyo unaweza kuitumia kwa yale muhimu zaidi kwako na ukafanikiwa sana.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kupeleka nguvu zako kwenye maeneo sahihi kwa mafanikio yako.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha