Kuna namba moja hatari sana kwenye maisha yako, namba hii ni hatari kwa chochote kile unachofanya, ni namba unayopaswa kuijua na kuiepuka kwa namna yoyote ile.

Namba hiyo ni namba moja. Namba moja, kwenye jambo lolote kwenye maisha ni namba hatari.

Unapoweka mategemeo yako yote kwenye kitu kimoja, unajiweka kwenye hatari ya kuangushwa, kukosa na hata kushindwa. Kutegemea kitu kimoja ni hatari kubwa sana, kwa sababu chochote kinachotokea kinavuruga mipango yako yote.

Kutegemea chanzo kimoja cha kipato kwenye maisha yako ni hatari kubwa sana, kwa sababu chochote kinachotokea kwenye chanzo hicho, kinakuweka kwenye wakati mgumu sana kifedha.

Kutegemea mteja mmoja kwenye biashara yako ni hatari kubwa sana, kwa sababu mteja huyo akiondoka biashara yako itayumba sana. Na hata yeye akijua unamtegemea yeye tu, anaweza kukusumbua kwa kukutaka ufanye anavyotaka yeye.

Kutegemea njia moja au mfumo mmoja kwenye chochote unachofanya kwenye maisha ni hatari kubwa. Kwa sababu siyo kila kitu huwa kinaenda kama tulivyopanga, hivyo ni muhimu kuwa na njia mbadala kwa chochote tunachofanya.

Namba moja ni namba hatari kwenye maisha yako, kazana kuikwepa namba hii ili uepuke kuanguka na kushindwa kwenye chochote unachofanya. Kuwa na njia mbadala, kuwa na tegemeo zaidi ya moja ili chochote kinachotokea kisiwe kikwazo kikubwa kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha