Mafanikio madogo yamekuwa kikwazo kikubwa kwa wengi kufikia mafanikio makubwa. Watu huwa wanaanza safari ya mafanikio wakiwa na hamasa kubwa, wakiwa tayari kujitoa zaidi na kuchukua hatua hatari ili kupata kile wanachotaka. Wanakuwa hawana cha kupoteza na hivyo hakuna kinachoweza kuwazuia.

Kwa namna hii wanavyoanza, inawasukuma sana kupiga hatua kubwa kwenye maisha yao, inawafanya kufanya yale ambayo kwa kawaida siyo rahisi kufanyika. Kwa kufanya huko hayo ambayo hayajazoeleka, kunawafanya wapate matokeo makubwa tofauti na walivyozoea.

Na hapo ndipo hatari inapoanzia, pale wanapopata matokeo makubwa tofauti na walivyozoea, wanabadilika, badala ya kushambulia kama walivyoanza, wanaanza kulinda. Badala ya kwenda na hamasa ya mwanzo, wanapunguza hamasa na kuacha kuchukua hatua hatari.

Hapa ndipo wengi huanguka na kurudi chini kabisa, hapa ndipo wengi hushindwa kuendelea kukua zaidi kwenye mafanikio.

Rafiki, pale unapofikiri umemaliza, ndiyo wakati sahihi wa kuanza,

Pale unapofikiri umeshafika juu kabisa, ni wakati wa kuanza kupanda juu zaidi.

Pale unapofikiri tayari unajua kila kitu, ndiyo wakati wa kuanza kujifunza upya.

Pale unapofikiri unaweza kufanya kila kitu, ndiyo wakati wa kuanza kufanya vile ambavyo hujawahi kufanya.

Pale unapofikiri huna haja ya kufanya chochote, ndiyo wakati wa kuanza kufanya kila kilicho muhimu na kwa umakini zaidi.

Na pale unapofikiri kwamba tayari una kila kitu, ndivyo wakati wa kuona kwamba bado hujawa na chochote.

Rafiki, kwa vyovyote vile, usikubali mafanikio kidogo unayopata yabadili mtazamo na fikra zako kwenye maisha. Usikubali mafanikio kidogo unayopata yawe sababu ya wewe kuanguka.

Ndiyo maana unahitaji kuwa na ndoto kubwa sana, ndoto ambazo unazifanyia kazi kila siku na unakazana kuwa bora zaidi kila siku.

Usiishi siku yoyote kwa mazoea, ishi kila siku kama siku mpya na kama siku ya mwisho kwako na hakuna siku ambayo haitakuwa na umuhimu kwako.

Maisha yako yana hatua mpya za kupiga kila siku, maisha yako yana mambo mapya ya kujaribu kila siku, na hatua yoyote uliyopiga sasa, ni ndogo sana ukilinganisha na hatua kubwa zaidi unazoweza kupiga.

Mafanikio yoyote uliyonayo sasa, ni madogo sana ukilinganisha na mafanikio makubwa zaidi unayoweza kufikia kwenye maisha yako.

Ndani yako bado upo uwezo mkubwa sana, uwezo ambao huwezi kumaliza kuutumia hata kama ungefanya nini. Usijiridhishe haraka na mafanikio madogo unayopata, kwa sababu haya yatakuwa sumu kubwa kwenye mafanikio makubwa zaidi unayoweza kuyafikia.

Na pia usidanganyike kwamba mafanikio yapo sehemu nyingine tofauti na hapo ulipo sasa, mafanikio makubwa yapo hapo hapo ulipo, unachohitaji ni kuchimba zaidi, kwenda ndani zaidi, kufanya zaidi, kujifunza zaidi na kujituma zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha